Pambazuko FM Radio

DC Kilombero Atoa Mwezi mmoja Wavamizi Hifadhi ya Ndefi kuondoka

7 November 2026, 14:03

Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Kilombero ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya Wakili Dunstan Kyobya (Mwenye Shati ya Bluu na Kofia Nyeusi Kulia) wakiwa kwenye Hifadhi ya Ndefi Kijiji cha Utengule Halmashauri ya Mlimba picha na Kuruthum Mkata

watu hawafuati taratibu zinazowekwa na Serikali hivyo waliovamia Hifadhi ya Ndefi watoke mara moja na Kambi zote zilizopo ndani ya hifadhi hiyo zivunjwe na kuondolewa-DC Kyobya

Na Kuruthum Mkata

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, amewataka wananchi waliovamia Hifadhi ya Ndefi iliyopo Kata ya Utengule Halmashauri ya Mlimba, ndani ya Pori la Akiba Kilombero, kuondoka mara moja na kuvunja kambi zao zote.

Hayo Amezungumza alipotembelea hifadhi hiyo,ambapo amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakikaidi utaratibu wa Serikali kuhusu uhifadhi, hivyo amesisitiza wote walio ndani ya hifadhi hiyo kuondoka hata hivyo amewaagiza viongozi wa Halmashauri hiyo kukaa pamoja na wananchi hao na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa uhifadhi.

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Wakili Dunstan Kyobya akisisitiza onyo alilolitoa mbele ya Wavamizi ndani ya Hifadhi ya Ndefi Picha na Kuruthum Mkata

sauti ya DC Kyobya

Naye Afisa Uhifadhi Mwandamizi wa TAWA Kilombero, Bedui Mboto, amesema shughuli za wananchi hao zimeathiri uoto wa asili. Hata hivyo, TAWA inaendelea na juhudi za kurejesha uoto huo, huku ikiahidi kutekeleza maagizo ya Mkuu wa Wilaya kwa kuhakikisha wananchi wanatoka na kambi zote zinavunjwa ndani ya mwezi mmoja.

Afisa Uhifadhi Mwandamizi wa TAWA Kilombero, Bedui Mboto, akisistiza Jambo ndani ya Hifadhi ya Ndefi Kijiji cha Utengule picha na Kuruthum Mkata

sauti ya Mhifadhi Mboto

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Utengule Anthony Mnyagani, ameiomba Serikali kuwapatia wananchi hao eneo la ardhi kutokana na ongezeko la watu, akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza na kuzuia migogoro ya muda mrefu.

Diwani wa Kata ya Utengule Anthony Mnyagani, akizungumza mbele ya kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kilombero picha na Kuruthum Mkata

sauti ya Diwani wa Utengule

Aidha Mwenyekiti wa Kijiji cha Utengule, Amos Kashinje, amesema kijiji kiko tayari kutoa elimu kwa wananchi ili waondoke ndani ya hifadhi hiyo. Hata hivyo, ameomba Serikali kutafuta suluhisho la kudumu kwa mgogoro huo, ikiwemo kuwapatia wananchi eneo la makazi ili kuimarisha uhifadhi na kuondoa migogoro.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Utengule, Amos Kashinje, akizungumza mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kilombero

sauti ya Mwenyekiti wa kijiji