Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
17 November 2026, 12:51

Viongozi wanaoingiza Wafugaji katika maeneo ya Vitongoji, Vijiji na Kata wachukuliwe hatua,na wale wanaofanya maeneo ya malisho kuwa makazi waondolewe mara moja-DC Kilombero.
Na Kuruthum Mkata
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, ameiagiza mamlaka husika kuwachukulia hatua viongozi wanaoshiriki kuwaingiza wafugaji katika vijiji bila kufuata taratibu za matumizi ya ardhi.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Ushauri la Wilaya kilichofanyika Ukumbi wa Mlimba, Kibaoni, Ifakara, Kyobya amesema maeneo ya malisho yanapaswa kuhakikiwa upya na walioyavamia kuondolewa kupitia operesheni maalumu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Bi. Pilly Kitwana, amesema halmashauri itaendelea kushirikiana na mamlaka nyingine kudhibiti uvamizi wa maeneo ya malisho, huku ikipanga kuongeza faini kwa wafugaji wanaokiuka taratibu, ambapo ng’ombe mmoja hutozwa shilingi laki moja kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.
Naye Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Kilombero, Seleman Vasomana, amesema baadhi ya wafugaji wamekuwa wakitumia maeneo ya malisho kama makazi, huku idadi ya mifugo ikiendelea kuongezeka na kuzidi uwezo wa maeneo yaliyotengwa, hivyo kuzitaka mamlaka kuchukua hatua za kudhibiti hali hiyo.

Kwa upande wao, baadhi ya watendaji wa kata wameeleza kukabiliwa na changamoto mbalimbali katika kusimamia shughuli za wafugaji, ikiwemo kupigwa bakora wanapotekeleza majukumu yao pamoja na ongezeko la mifugo katika maeneo wanayoyasimamia.