Pambazuko FM Radio

Uyoga kuongeza kipato Kilombero

25 November 2026, 21:58

Picha ya baadhi ya wanakikundi waliopatiwa mafunzo(Picha kwa hisani ya STEP)

Wanakikundi wamepatiwa mafunzo ya vitendo ya wiki mbili kuhusu uzalishaji wa uyoga, kuanzia maandalizi ya vifaa, mifuko ya kuoteshea hadi namna ya kutunza na kusimamia ukuaji wake.

Na Katalina Liombechi

Shirika la Southern Tanzania Elephant Program (STEP), kwa kushirikiana na Prime Mushroom Tanzania, limewezesha kikundi cha Tembo wa Milesa (TEWAMI) kuanza uzalishaji wa uyoga kama njia mbadala ya kujipatia kipato na kuimarisha uchumi wa kaya katika Bonde la Kilombero, kupitia ufadhili wa Polish Aid.

Kikundi hicho kilichopo Kijiji cha Kanyenja kina wanachama 36, ambapo asilimia 53 ni wanawake na asilimia 83 ni vijana.

Kwa mujibu wa Mratibu wa mradi huo Catherine Kimario kutoka STEP amesema Wanachama hao wamepatiwa mafunzo ya vitendo ya wiki mbili kuhusu uzalishaji wa uyoga, kuanzia maandalizi ya vifaa, mifuko ya kuoteshea hadi namna ya kutunza na kusimamia ukuaji wake.

Katika utekelezaji wa mpango huo, pia limejengwa banda maalumu la kuzalishia uyoga na kuandaliwa mifuko 100 ya kuoteshea, hatua inayolenga kuwawezesha wanachama kuanza uzalishaji na baadaye kuuza mazao hayo katika masoko ya ndani.

Mpango huo unatajwa kuwa fursa muhimu kwa wakazi wa Bonde la Kilombero kupanua vyanzo vya mapato na kupunguza utegemezi wa kilimo pekee, hususan kutokana na changamoto za uharibifu wa mazao unaosababishwa na tembo pamoja na athari nyingine zinazoathiri shughuli za kilimo.

Kupitia mpango huo, STEP inalenga kuimarisha ujasiriamali, kuongeza ustahimilivu wa kiuchumi wa jamii na kukuza shughuli endelevu za kujipatia kipato, sambamba na kuendeleza juhudi za uhifadhi wa mazingira na wanyamapori katika Bonde la Kilombero.

Picha ya Wanakikundi wakifuatilia mafunzo(Picha na STEP)

Tumewapatia wanachama mafunzo ya vitendo ya wiki mbili kuhusu uzalishaji wa uyoga, tukajenga banda maalumu na kuandaa mifuko 100 ya kuoteshea, ili kuwawezesha kujipatia kipato kupitia uzalishaji na uuzaji wa uyoga, kupunguza utegemezi wa kilimo pekee na kuimarisha uhifadhi wa mazingira na wanyamapori katika Bonde la Kilombero.