Pambazuko FM Radio

Jukwaa lafichua kero sekta ya ushirika Morogoro

24 June 2026, 19:56

Picha ya DC Kyobya na wana ushirika Morogoro kwenye kongamano la jukwaa(Picha na Katalina Liombechi)

Viongozi na watendaji wa ushirika watakiwa kuchukua hatua madhubuti za kuzuia vitendo vya rushwa ili kuongeza ufanisi katika utendaji na kuimarisha imani ya wanachama

Na Katalina Liombechi

Uwepo wa baadhi ya watendaji na wajumbe wa bodi wasio waaminifu pamoja na ubovu wa miundombinu ya barabara imetajwa kuwa ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili sekta ya ushirika katika Mkoa wa Morogoro.

Hayo ni kwa mujibu wa mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Bertha Mwanzalima, amewasilisha taarifa kuhusu hali ya ushirika katika Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Morogoro 2026 ambalo linafanyika Ifakara kwa siku mbili kuanzia leo June 24,2026 katika ukumbi wa Vunjabei likiwa na lengo la kujadili fursa,mafanikio,changamoto na kuweka mikakati ya kukabiliana nazo ili kuongeza tija na mchango wa ushirika katika maendeleo ya wananchi.

Picha ya Bertha Mwanzalima(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya Bertha Mwanzalima

Mgeni rasmi katika ufunguzi wa jukwaa hilo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mheshimiwa Adam Malima.

Akijibu hoja na changamoto zilizowasilishwa, Wakili Dunstan Kyobya amesisitiza umuhimu wa kuzingatia weledi, uadilifu, uwazi na ushirikishwaji katika utoaji wa huduma kwa wanachama wa vyama vya ushirika huku akitaka viongozi na watendaji wa ushirika kuchukua hatua madhubuti za kuzuia vitendo vya rushwa ili kuongeza ufanisi katika utendaji na kuimarisha imani ya wanachama.

Aidha, Kyobya amesema Serikali imezipokea changamoto zilizowasilishwa na yuko tayari kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuzitafutia ufumbuzi kwa kushirikiana na wakuu wa wilaya zingine ndani ya Mkoa wa Morogoro katika kushughulikia baadhi ya changamoto za pamoja, ikiwemo migogoro ya matumizi ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji ambayo imekuwa ikiathiri shughuli za uzalishaji na maendeleo ya ushirika.

Picha ya DC Kyobya(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya DC Kyobya

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Grace Masambaji, amesema baadhi ya changamoto zinazojitokeza katika vyama vya ushirika zinatokana na utendaji wa viongozi wenyewe, hivyo ni muhimu viongozi hao wawajibike kwa matendo yao na kuzingatia misingi ya utawala bora katika usimamizi wa vyama wanavyoongoza.

Picha ya Grace Masambaji(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya Grace Masambaji

Jukwaa hilo linalofanyika chini ya kauli mbiu isemayo “Ushirika kwa dunia yenye amani: linda ushirika, chagua uadilifu.” linatarajiwa kutoa fursa kwa washiriki kubadilishana uzoefu, kujadili mbinu bora za kuimarisha ushirika na kuweka mikakati ya pamoja itakayochochea maendeleo ya sekta hiyo katika Mkoa wa Morogoro na nchini kwa ujumla.