Pambazuko FM Radio

Vijana 1,345 Kilombero wanufaika mradi wa SET

22 May 2026, 20:24

Picha ya Vijana wanufaika Mradi wa SET(Picha na Katalina Liombechi)

vijana wanaowezeshwa na shirika la Swisscontact ni wenye umri kati ya miaka 15-24 na kwamba asilimia 80 ya walionufaika kwa awamu hii ni wasichana

Na Katalina Liombechi

Shirika la Swisscontact limefanikiwa kuwawezesha vijana 1,345 wa kike na kiume katika Wilaya ya Kilombero kupitia mradi wa Skills for Employment Tanzania (SET) chini ya ufadhili wa Serikali ya Uswiss kupitia ubalozi wake nchini Tanzania, ili waweze kujitegemea kiuchumi.

Akizungumza katika Tamasha la maonesho ya biashara ya vijana wanufaika wa mradi huo ambayo yamefanyika katika Halmshauri ya Mji wa Ifakara kwa siku mbili Mei 21-22,2026  Meneja wa Mafunzo wa mradi wa SET, Victoria Nkuba,amesema vijana wanaowawezesha ni wenye umri kati ya miaka 15-24 na kwamba asilimia 80 ya walionufaika kwa awamu hii ni wasichana.

Amesema mradi huo unatekelezwa chini ya kauli mbiu isemayo “Tunatengeneza fursa za kujitegemea kwa vijana.”

Picha ya Meneja wa Mafunzo wa mradi wa SET, Victoria Nkuba(Picha na Katalina Liombechi)

Sauti ya Meneja wa Mafunzo wa mradi wa SET, Victoria Nkuba

Mgeni rasmi katika hafla hiyo Witness Kimoleta Afisa Elimu Msingi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya  amelipongeza shirika hilo kwa mradi huo ambao umegusa maisha ya vijana huku akitoa wito kwa vijana hao kuyatumia mafunzo na ujuzi waliopatiwa kujinufaisha wenyewe na jamii wanazotoka.

Amesema Serikali ya Tanzania kupitia Wizara yenye dhamana ya vijana ina nia njema ya kufungua fursa kwa vijana kwa kuruhusu mashirika kama Swisscontact kufanya kazi nchini na kuwainua kiuchumi.

Picha ya Mwalimu Witness Kimoleta Afisa Elimu Msingi Halmashauri ya Mji wa Ifakara(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya Mwalimu Witness Kimoleta Afisa Elimu Msingi Halmashauri ya Mji wa Ifakara

Kwa upande wao, wanufaika wa mradi huo wameeleza kushukuru kwa kupata mafunzo ambayo yamewasaidia kuwainua kiuchumi na kujitegemea baada ya kutoka katika mazingira magumu ya maisha.

Picha ya Mgeni rasmi akikagua kazi za Vijana wanufaika wa mradi wa SET(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti za Vijana Wanufaika mradi wa SET

Wakati huu mradi wa SET unapoelekea mwishoni umesaidia vijana hao kwa kuwapatia ujuzi wa fani mbalimbali kama ushonaji,usindikaji wa mchele Joto,kuanzishiwa biashara mbalimbali ili waweze kujitegemea huku jamii ikiombwa kuwaunga mkono vijana hao ili waweze kufanikiwa zaidi.