Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
21 April 2026, 18:58

kupitia vifurushi hivyo, wanachama wanaweza kupata huduma za matibabu katika vituo mbalimbali vya afya vilivyosajiliwa, jambo linalorahisisha upatikanaji wa huduma hizo bila gharama kubwa ya papo kwa papo
Na Katalina Liombechi
Jamii imetakiwa kuchukua hatua madhubuti za kujihakikishia huduma bora za matibabu pale wanapougua kwa kukata bima ya afya ya NHIF, ikiwa ni mkakati wa Serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya bila usumbufu.
Hayo yameelezwa na Msimamizi wa NHIF anayehudumia wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi, Salma Marijani, alipokuwa akizungumza na Pambazuko FM leo Aprili 21, 2026 katika Ofisi yake iliyopo Kata ya Kibaoni Ifakara.
Amesema kuwa bima ya NHIF imeboreshwa na haina usumbufu, kwani ina vifurushi mbalimbali vinavyokidhi mahitaji ya makundi tofauti ya wananchi.
Bi. Marijani amefafanua kuwa kupitia vifurushi hivyo, wanachama wanaweza kupata huduma za matibabu katika vituo mbalimbali vya afya vilivyosajiliwa, jambo linalorahisisha upatikanaji wa huduma hizo bila gharama kubwa ya papo kwa papo.
Aidha, amesema kwa sasa NHIF inaendelea na kampeni ya fao la toto afya card ya Tsh.50400/= kampeni inayoendana na kutoa elimu kwa katika shule na maeneo mbalimbali ili jamii kuwahamasisha wananchi kujiunga na bima hiyo.
Lengo la kampeni hiyo ni kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa bima ya afya na namna inavyoweza kusaidia kupunguza changamoto za kifedha wakati wa matibabu.
Amesisitiza kuwa ushiriki wa wananchi katika kujiunga na NHIF ni hatua muhimu ya kujenga jamii yenye afya bora na yenye uwezo wa kukabiliana na gharama za matibabu kwa ufanisi.
