Pambazuko FM Radio

Wamiliki wa Matrekta Wapongeza Polisi Kilombero

25 July 2026, 13:58

washiriki wa mafunzo kwa wamiliki na madereva wa Matrekta na Power Tiller – picha na: WP13369 PC Janeth

Wamiliki na madereva wa matrekta na power tiller tarafa ya Kidatu wilayani Kilombero wamepongeza jeshi la polisi kwa mafunzo ya usalama barabarani, huku wakipokea maelekezo ya kujiorodhesha ili kurahisisha utoaji wa mafunzo na leseni katika eneo lao.

Na: Isidory Mtunda

Wamiliki wa Matrekta na Power Tiller Tarafa ya Kidatu wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro wamelipongeza jeshi la polisi wilayani humo, kupitia kitengo cha usalama barabarani, kwa kuwapatia mafunzo ya usalama barabarani yanayohusu vyombo vyao.

wamiliki na madereva wa Matrekta na Power Tiller Nyandeo wakiuliza maswali – picha na: WP13369 PC Janeth

Wakizungumza baada ya mafunzo yaliyotolewa na Mkuu wa Usalama Barabarani wa Wilaya ya Kilombero (DTO), mrakibu msaidizi wa Polisi (SP) Blandina Kasongwa na timu yake, washiriki hao wamesema mafunzo hayo yanapaswa kuendelea kutolewa mara kwa mara. Wameomba pia kuandaliwa kwa utaratibu maalum wa kupatiwa mafunzo hayo kwa pamoja ndani ya tarafa yao ili kuwawezesha madereva kupata leseni kwa urahisi.

Sauti za wananchi

Akijibu maombi ya washiriki hao, DTO Kasongwa amewaagiza madereva na wamiliki wa matrekta kujioredhesha ili kubaini idadi yao na utayari wao, kisha kuwashirikisha wakuu wa vituo vyao vya polisi. Hatua hiyo itamwezesha DTO kwa kushirikiana na mkuu wa Usalama Barabarani wa Mkoa (RTO) kuchukua hatua ya kuwaita wakufunzi kwa ajili ya kuja kutoa mafunzo moja kwa moja katika tarafa hiyo.

DTO Kilombero B. Kasongwa – picha na:WP13369 PC Janeth
Sauti ya DTO B. Kasongwa

Naye Mkaguzi wa Magari na Mtoaji wa Leseni wilaya ya Kilombero, Sajenti Rajabu Juma Kadikarange, amewashauri madereva hao kwamba baada ya kujiandikisha, waandike barua kwa vyuo vinavyotoa mafunzo ili vifike Tarafa ya Kidatu kutoa mafunzo hayo, badala ya wao kulazimika kusafiri hadi Morogoro kufuata huduma hiyo.

Sauti ya mkaguzi wa magari Sajenti R. Kadikarage

Kwa upande wake, Mkuu wa Kituo cha Polisi Kidatu, Sajenti Wami E. Matonya, amewaaasa madereva hao kuacha tabia ya kuendesha vyombo vya moto wakiwa wamelewa, kuepuka tabia hatarishi ya kuchanganya mazao na abiria kwenye tela za matrekta, pia waache  kukokota majembe kwenye barabara za lami kwani vitendo hivyo vinahatarisha usalama wa abiria na kuharibu miundombinu.