Pambazuko FM Radio

DC Kilombero: Zingatia matumizi sahihi uhifadhi mazingira

7 June 2023, 10:09 am

Wananchi wa kijiji cha Chiwachiwa – siku ya Mazingira dunia – Picha na Katalina Liombechi

“Nawaagiza wananchi wa kijiji cha Chiwachiwa pamoja na  viongozi kutunza na kuhakikisha miti 500 iliyopandwa katika shule ya msingi Chiwachiwa inakua”. Mkuu wa wilaya ya Kilombero Wakili Dunstan Kyobya

Na; Katalina Liombechi

Imeelezwa kuwa katika kijiji cha Chiwachiwa halmashauri ya Mlimba bado kuna changamoto za utekelezaji wa shughuli za uhifadhi wa mazingira kutokana na kutozingatia matumizi bora ya ardhi na kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo yaliyohifadhiwa.

Afisa Mtendaji kijiji cha Chiwachiwa akisoma risara mbele ya DC Kyobya – Picha na Katalina Liombechi

Hayo yamesemwa na afisa mtendaji wa kijiji hicho Bwana Basili Mwaka wakati akisoma risala kwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya mazingira duniani ambapo wilayani Kilombero yamefanyika  katika kijiji cha Chiwachiwa halmashauri ya Mlimba.

Sauti ya afisa mtendaji wa kijiji – bwana Basil Mwaka

Mgeni rasmi mkuu wa wilaya ya Kilombero Wakili Dunstan Kyobya amekemea shughuli zinazoharibu mazingira huku akitoa wito kwa jamii kuacha mara moja huku akieleza kuwa mto Kilombero unategemewa kupeleka asilimia 65 ya maji yake katika mradi mkubwa wa uzalishaji umeme Bwawa la Mwalimu Nyerere hivyo anayefanya uharibifu katika vyanzo vya maji anahujumu mradi huo.

DC Kyobya akipanda mti – Picha na; Katalina Liombechi

Hata hivyo ametoa wito kwa wananchi wa kijiji hicho na kuwaagiza viongozi kutunza na kuhakikisha miti 500 iliyopandwa katika Shule ya Msingi Chiwachiwa inakuwa.

Sauti ya Dc wa Kilombero Danstan Kyobya

Meneja wa shirika linalojihusisha na uhifadhi wa wanyamapori Afrika AWF Clarence Msafiri amesema wao wanaamini kuwa mifumo ya Ikolojia na Bionuai ndio msingi wa afya na maendeleo ya jamii hivyo kuna kila sababu ya jamii kutambua na  kuwa waangalifu na shughuli wanazozifanya ili kunusuru mifumo hiyo kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Sauti ya Meneja wa AWF – C. Msafiri

Diwani wa kata hiyo Nestory Kyerula na baadhi ya wananchi akiwemo Asunta Gabriel na mwanafunzi Grace Samuel wameshukuru ujio wa mkuu wa wilaya pamoja na kuamua kufanya maadhimisho hayo katika kijiji chao huku wakiahidi kuitunza miti iliyopandwa na kuendeleza shughuli za uhifadhi kwa kushirikiana na wadau.

sauti ya diwani na wananchi wa kijiji cha Chiwachiwa