Pambazuko FM Radio

Ujenzi wa Mabwawa ya kuvuna maji ya mvua yatasaidia kuondoa Mafuriko- Ifakara

3 April 2024, 11:58 am

Picha hii inaonyesha hali inavyokuwa Ifakara msimu wa masika ambapo huwa inaathiriwa na Mafuriko kila mwaka {Picha kutoka maktaba ya Pambazukofm}

“Maelekezo ya Mh Rais Samia Suluhu Hassani kwa Wizara ya maji na sekta zake ni kuhakikisha wanajenga mabwawa ya kimkakati ya kuvuna maji ya mvua ili kuzuia mafuriko”=Waziri wa Maji Mh,Juma Aweso

Na Elias Maganga

Wizara ya maji imesema leo bungeni Jijini Dodoma kuwa itahakikisha inajenga mabwawa ya kimkakati ya kuvuna maji ya mvua ili kuondokana na adha ya mafuriko ambayo imekuwa ikiwakumba mara kwa mara wakazi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara Wilayani Kilombero.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Waziri wa Maji Mheshimiwa Juma Aweso wakati akijibu swali la nyongeza kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Kilombero Mh,Abubakar Asenga aliyehoji ni lini serikali itafanya mradi wa kuvuna maji ya mvua na kuboresha Mto Lumemo ili kupunguza adha ya mafuriko kwa wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara.

Picha ya Mbunge wa Jimbo la Kilombero Mh Abubakar Asenga akiwa Bungeni Dodoma{Picha kwa Hisani ya Mustafa shujaa}
Sauti ya Mbunge wa Jimbo la Kilombero Mh Abubakar Asenga

Akijibu Swali hilo Waziri wa Maji Mheshimiwa Juma Aweso ameliambia Bunge kuwa kwa maelekezo waliyopewa na Mheshimiwa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ni kujenga mabwawa ya kimkakati na tayari wameshaanza baadhi ya mabwawa na pia wamepewa mitambo ya uchimbaji na ifakara itapewa kipaumbele katika uchimbaji wa mabwawa hayo

Picha ya Waziri wa Maji Mheshimiwa Juma Aweso
Sauti ya Waziri wa Maji Mheshimiwa Juma Aweso