Pambazuko FM Radio

Tembo wachangia maendeleo -Ifakara

27 May 2023, 12:03 pm

Kundi la Tembo {Picha kwa hisani ya Getty Images}

Kutokana na wananchi wa Kijiji cha Sole kata ya Mkula Halmashauri ya Mji wa Ifakara kutembea umbali mrefu kufuata huduma za Afya,STEP,imekabidhi hundi ya kiasi cha Shilingi Mil 10 ,kwa ajili ya Ujenzi wa Zahanati ya Kijiji hicho hali itakayosaidia wananchi hao kuondokana na adha hiyo.

Na Katalina Liombechi

Shirika linalojihusisha na Uhifadhi wa Tembo kusini mwa Tanzania(STEP) wamekabidhi hundi ya kiasi cha Shilingi Mil 10 katika Kijiji cha Sole Kilichopo Kata ya Mkula Halmashauri ya Mji wa Ifakara kwa ajili ya Ujenzi wa Zahanati ya Kijiji hicho hali itakayosaidia wananchi hao kuondokana na Adha ya kutembea Umbali Mrefu kufuata huduma za afya katika maeneo mengine.

Akizungumza wakati wa kusaini Mkataba huo kati ya Kijiji hicho na STEP Meneja wa Shirika hilo Joseph Mwalugelo amesema lengo la kusaini Mkataba huo ni kudumisha mahusiano ya  ujirani Mwema wa kurudisha kwa jamii,kufanya wananchi kuguswa moja kwa moja na suala la uhifadhi wa Tembo na kulinda ushoroba.

Aidha amesema hiyo inakuja baada ya Baadhi ya Wananchi kujitolea maneo yao kwa ajili ya uhifadhi hivyo STEP wameona Jamii nzima pia wanufaike kupitia uhifadhi huo na kufahamu umuhimu wa uwepo wa Tembo.

Mwalugelo Amesema hiyo inaupa nguvu Uhifadhi kwani jamii hiyo itaona uhusiano wa tembo na Maendeleo yao.

Meneja wa Shirika la STEP Joseph Mwalugelo {Picha na Katalina Liombechi}

Katika hatua nyingine Meneja huyo amesema STEP wamekuwa wakihamasisha shughuli za Kiuchumi ambazo ni rafiki kwa Mazingira ikiwa ni pamoja na Ufugaji wa Nyuki kwenye mipaka ya Hifadhi kwa maendeleo endelevu ya Rasilimali hiyo ambapo kupitia shughuli hiyo wananchi wananufaika kiuchumi sambamba na kuhifadhi mazingira.

Sauti ya Meneja wa Shirika la STEP Joseph Mwalugelo

Kwa Upande wao Diwani wa Kata hiyo ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mh Andrew Matajiri na Mwenyekiti wa Kijiji Hicho Michael Makalanga wameelezea sababu za kufikiria Mradi wa Zahanati ni kutokana na wananchi kuona changamoto za huduma hizo kwani wamekuwa wakizifuata katika Kijiji cha Sonjo Mang’ula huku wakiahidi kutzitumia fedha hizo kwa matumizi kusudiwa sambamba na kushirikiana na STEP kuendelea kuhifadhi Tembo.

Diwani wa Kata ya Mkula ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara hiyo Mh, Andrew Matajiri {Picha na Katalina Liombechi}

Sauti ya Diwani wa Kata ya Mkula ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mh Andrew Matajiri na Mwenyekiti wa Kijiji cha Sole Michael Makalanga

Wakizungumza Baadhi ya Wananchi wa Kijiji hicho akiwemo Veronika Kiputa,Said Mkondoa na Osward Senyagwa Wameishukuru STEP kwa kuwajali na kuwapatia fedha hizo ambapo Ujenzi wa zahanati utakapokamilika watafurahia kupata huduma za kiafya katika kijiji chao kwani wanapata changamoto nyingi kuzifuata huduma za kiafya katika maeneo mengine hasa wanapohitaji matibabu nyakati za Usiku.

Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Sole{Picha na Katalina Liombechi}

Aidha kutokana na STEP kutekeleza jambo hilo wao kama wananchi watakuwa Mabalozi wa kuelezea Umuhimu wa Tembo katika kuunga mkono shughuli za Maendeleo na kuendeleza Ushoroba.

Sauti za baadhi ya Wananchi wakielezea kuwa wao watakuwa Mabalozi wa kuelezea Umuhimu wa Tembo

Shirika la STEP Wamekuwa wakijenga Uhusiano huo kati ya Mnyama Tembo na Jamii ambapo kiasi kama hicho pia wamekitoa katika Kijiji cha Kanyenja,Kijiji cha Sole na wanatarajia kupeleka kiasi hicho pia katika kiji cha Mang”ula A ili kuzipa nguvu jamii hizo kuhifadhi Tembo.