Pambazuko FM Radio

Timu ya Msolwa Station yaibuka bingwa-Tembo cup

7 July 2023, 5:09 pm

Timu yenye Jezi ya Blue ni Msolwa stationi na yenye jezi ya Kijani ni Mang’ula B wakionyesha uwezo katika fainali za Tembo Cup {Picha na Katalina Liombechi}

Na Katalina Liombechi

Mashindano ya Kilombero Tembo Cup yamemalizika kwa Msimu huu wa Mwaka 2023 baada ya Fainali iliyokutanisha Timu ya Msolwa Station kuibuka na Ushindi wa Mabao 5-4 dhidi ya Mang’ula B ushindi ambao umepatikana kwa Mikwaju ya Penati.

Mashindano hayo yalihusisha takribani Timu 12 kutoka katika vijiji vilivyopitiwa na Mapito ya Tembo katika Tarafa ya Mang’ula Halmashauri ya Mji wa Ifakara na  Fainali imechezwa katika Viwanja vya Shule ya Msingi Mang’ula A.

Katika Mashindano hayo Mshindi wa Kwanza ameondoka na Kombe pamoja na Kiasi cha Shilingi Laki saba na Mpira, huku mshindi Wa pili akiondoka na zawadi ya shilingi laki Tano na Mpira na Mshindi wa Tatu amepata Kiasi cha shilingi laki Tatu na Mpira.

Meneja Mwendeshaji  kutoka STEP, bi Grace Kawogo{Picha na Katalina Liombechi}

Kwa mujibu wa Waandaaji wa Mashindano hayo Meneja mwendeshaji  kutoka STEP, bi Grace Kawogo amesema Lengo la mashindano hayo ni kuwakutanisha Vijana na Jamii kwa ujumla na kufikisha ujumbe wa kumlinda Tembo na kujenga Mahusiano mazuri kati ya watu na Mnyama huyo pamoja na kuwapa Elimu ya kufahamu namna ya kujikinga pale wanapokutana na Tembo kwa ajili ya kuendeleza uhifadhi.

Sauti ya Meneja mwendeshaji  kutoka STEP, Grace Kawogo

Upande wao Washindi wa Mchezo huo kutoka Timu ya Msolwa Station Keptain Dunstan Njoka na Mwalimu wa Timu hiyo Hassan Matata Maarufu kama Makoko wamesema siri ya ushindi ni maandalizi mazuri na Uchumi Imara wa Timu yao.

Kapteni wa Timu ya Msolwa Station Dunstan Njoka{Picha na Katalina Liombechi}
Sauti za Kapteni wa Msolwa Station Dunstan Njoka na Mwalimu wa Timu hiyo Hassan Matata

Hata hivyo kwa Upande wa Timu ya Mang’ula B Mchezaji Mohamed Mamba amesema haikuwa riziki yao licha ya kujituma uwanjani na kwamba wapinzani wao wametumia mapungufu yao kuwaadhibu katika Mikwaju ya Penati huku akiwashukuru STEP Kwa kuitisha Mashindano hayo yanayoibua vipaji kwa vijana.

Mchezaji wa Mang’ula B Mohamed Mamba{Picha na Katalina Liombechi}
Sauti ya mchezaji wa Mang’ula B, Mohamed Mamba

Mgeni Rasmi katika fainali hiyo alikuwa Afisa Mtendaji wa Kata ya Mwaya Bwana Acrey Mhenga naye akizungumza kwa Niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mh Dunstan Kyobya amesema Wilaya hiyo ina kila sababu ya kujivunia kuwa na vijana wenye vipaji mbalimbali na wenye utayari wa kushiriki Michezo.

Mgeni Rasmi katika fainali hiyo alikuwa Afisa Mtendaji wa Kata ya Mwaya Bwana Acrey Mhenga{Picha na Katalina Liombechi}
Sauti ya Mgeni Rasmi Afisa Mtendaji wa Kata ya Mwaya Bwana Acrey Mhenga

Mashindano hayo yaliyoanza June 18 yakihusisha Timu 12 na yametamatika kwa Fainali iliyochezwa na Timu za Msolwa station na Mang’ula B July 5 mwaka huu 2023 yaliandaliwa na Shirika linalojihusisha na Uhifadhi wa Tembo kusini mwa Tanzania STEP kwa ufadhili wa USAID.