Pambazuko FM Radio

Mikakati ya kuondokana na uchafu wa mazingira yaanza kutekelezwa-Ifakara

11 February 2023, 4:14 pm

Wananchi wakiwa kwenye zoezi la usafi eneo la stendi ya mabasi Ifakara{Picha na Elias Maganga}

Na Elias Maganga

Wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara Wilayani Kilombero wameshauriwa kuunga mkono kampeni ya usafi wa mazingira inayojulikana Usafi wangu mita tano na mita tano usafi wangu,kwa kufanya hivyo watakuwa wanajikinga dhidi ya  magonjwa mbalimbali ya maambukizi.

Wito huo umetolewa na Afisa Afya wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara Bwana Jafary Ngogomela alipokuwa akihamasisha usafi wa mazingira ambao hufanyika jumamosi ya kila wiki.

Bwana Ngogomela amesema  unapoimarishwa usafi wa mazingira jamii inajikinga na magonjwa ya maambukizi ambayo yanatokana na uchafu wa mazingira.

Aidha ametaja sababu zilizopelekea Mji wa Ifakara kuwa ni ya mwisho katika mashindano ya usafi wa mazingira Kitaifa, ikiwa ni pamoja na kuzagaa kwa taka,kuweka taka pembezoni mwa barabara na kutokuwa na vyoo bora.

Afisa afya wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara Bwana Jafary Ngogomela
Sauti ya Afisa afya wa Halmashauri ya Mji a Ifakara Bwana Jafary Ngogomela akielezea umuhimimu wa kufanya usafi

Kwa upande wake mwenyekiti wa stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani iliyopo kata ya Kibaoni katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara Bwana Farijala Mbena amesema kampeni hiyo imewasaidia kwani kwa sasa stendi hiyo ina muonekano mzuri kimazingira tofauti na zamani ambapo hali ya usafi ilikuwa ni mbaya.

Bwana Mbena amesema kwa sasa wanaandaa utaratibu wa kuweka vyombo vya kuhifadhia taka na kuwatangazia abiria kutotupa taka na badala yake wazihifadhi kwenye vyombo maalumu vya taka vitakavyowekwa katika stendi hiyo.

Mwenyekiti wa Stendi Ifakara Bwana Farijala Mbena {Picha na Elias Maganga}
Sauti ya Mwenyekiti wa Stendi ya mabasi Ifakara akielezea mikakati wanayoiweka ya usafi

Nao watumiaji wa stendi hyo waliokutwa na Pambazukofm wakifanya usafi wamepongeza utaratibu huo uliowekwa na Halmashauri ya Mji wa Ifakara na wameomba zoezi hilo liwe endelevu kwani litasaidia kuuweka mji katika hali ya usafi.

Wananchi waliojitokeza kufanya usafi {Picha na Elias Maganga}
Sauti za wananchi wakiomba zoezi hilo liwe endelevu

Ikumbukwe kampeni hii ya mita tano usafi wangu na usafi wangu mita tano, imekuja baada ya Halmashauri ya Mji wa Ifakara kuwa ya mwisho kwa usafi wa mazingira Kitaifa.