Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
4 June 2026, 20:15

shirika hilo limeahidi kupeleka mapipa mawili katika kambi hizo mbili ili kusaidia ukusanyaji na uhifadhi wa taka za plastiki kabla ya kupelekwa viwandani kwa ajili ya kurejelewa na kutumika tena
Na Katalina Liombechi
Katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayotarajiwa kufanyika Juni 5, 2026, Shirika la Six Rivers Africa kwa kushirikiana na Serikali leo limetoa elimu ya uhifadhi na usimamizi wa taka za plastiki katika kambi za uvuvi za Funga na Migude, ikiwa ni sehemu ya shughuli za kuadhimisha siku hiyo muhimu.
Mbali na kutoa elimu, shirika hilo pamoja na wananchi wa maeneo hayo wameshiriki kwa vitendo katika zoezi la usafi kwa kuondoa taka za plastiki ambazo zimekuwa tishio kwa uendelevu wa hifadhi ya jamii ILUMA na Mto Kilombero, maeneo yenye umuhimu mkubwa kiikolojia kutokana na mchango wake katika kuhifadhi bioanuwai na rasilimali za asili.
Akizungumza katika shughuli hiyo,Afisa nyuki wa Six Rivers Africa, Lucas Dege, amesema kuwa pamoja na kutekeleza miradi mbalimbali ya kuiunga mkono Serikali katika juhudi za uhifadhi wa mazingira, shirika hilo linaamini kuwa elimu, ushirikishwaji wa jamii na kuonyesha kwa vitendo namna bora ya kutunza mazingira ni njia muhimu ya kujenga utamaduni endelevu wa uhifadhi.
Amesema kuwa shirika hilo limeahidi kupeleka mapipa mawili katika kambi hizo mbili ili kusaidia ukusanyaji na uhifadhi wa taka za plastiki kabla ya kupelekwa viwandani kwa ajili ya kurejelewa na kutumika tena.

Kwa upande wake, Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Salome Mayenga, amesema hatua hizo ni njia bora ya kushirikisha jamii kutambua umuhimu wa kulinda maeneo hayo muhimu ya kiikolojia.
Amebainisha kuwa uharibifu wa mazingira unaweza kusababisha athari kubwa kwa maisha ya watu pamoja na viumbe hai wengine wakiwemo samaki na wanyamapori.
Aidha, Bi. Mayenga ametumia fursa hiyo kuwaalika wananchi kushiriki kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yatakayofanyika Juni 5, 2026 katika Kijiji cha Kining’ina.
Amesema maadhimisho hayo yatahusisha zoezi la upandaji miti zaidi ya 5000 kando ya Mtuo Lumemo pamoja na majadiliano kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ifakara kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira.
Ameeleza kuwa shughuli hizo zinalenga kujenga dhana ya urithishaji wa rasilimali za mazingira kwa vizazi vijavyo, kuongeza uelewa kuhusu masuala ya uhifadhi, pamoja na kuimarisha juhudi za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Naye Kiongozi wa Kambi ya Uvuvi ya Migude, Godfrey Mwakabana, amewashukuru Six Rivers Africa kwa elimu na ushirikiano walioutoa katika kusafisha maeneo hayo huku wakiahidi kuendeleza utaratibu wa kufanya usafi kila Jumamosi ili kujilinda wenyewe na kulinda wanyama wanaopatikana katika hifadhi hizo.

Siku ya Mazingira Duniani huadhimishwa kila mwaka ifikapo Juni 5 na Kauli mbiu kwa mwaka 2026 nchini Tanzania ni:
“Tuwajibike Kukijanisha Tanzania.”