Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
3 August 2026, 23:12

Polisi wilayani Kilombero wamewataka madereva wa bodaboda na bajaji kuzingatia sheria za usalama barabarani, huku madereva wakiiomba Serikali kuwasogezea mafunzo ya leseni na kuboresha utambuzi wa vyombo vyao.
Na; Isidory Mtunda
Baadhi ya madereva wa vyombo vya moto wametajwa kuendelea kukiuka sheria za usalama barabarani kwa kutovaa kofia ngumu (helmet), kuendesha wakiwa wamelewa, kutumia simu wanapoendesha, pamoja na kubeba mizigo au abiria kinyume cha sheria. Hayo yamesemwa na Polisi Kata wa Sanje, Inspekta Godfrey Sambu, wakati wa kikao cha madereva wa bodaboda na bajaji wa Tarafa ya Kidatu kilicholenga kuhamasisha ulipaji wa ushuru wa halmashauri kupitia ukataji wa stika za pikipiki na bajaji.
Kwa upande wao, madereva hao wamelalamikia baadhi ya wenzao kukataa kujiunga na vikundi vya madereva, hali inayowafanya wateja kushindwa kupata msaada wanaposahau mizigo kwenye bajaji. Pia wamemuomba Ofisa wa Usalama Barabarani (DTO) kuratibu mafunzo ya leseni katika kata yao ili kuwawezesha kupata leseni halali na kuondokana na changamoto ya kukwepa askari wa usalama barabarani.
Nao viongozi wa madereva hao, Mohamedi Ishikala na Jimmy Lipingu, wamesema tayari wameanza kutekeleza utaratibu wa kuweka nembo maalumu kwenye bajaji, zitakazoonesha utambulisho wa Wilaya ya Kilombero pamoja na namba ya kituo cha maegesho, hatua wanayoamini itarahisisha utambuzi wa vyombo hivyo na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Usalama Barabarani Wilaya ya Kilombero (DTO), ASP Blandina Benedict Kasongwa, amewapongeza madereva kwa kuunda vikundi na kuwataka wanaohitaji mafunzo ya leseni kujiorodhesha ili kurahisisha uratibu wa wakufunzi na kuwawezesha kupata leseni kwa kufuata taratibu za kisheria.