Pambazuko FM Radio

Polisi yapiga marufuku double parking Ifakara

16 August 2026, 12:57

Baadhi ya wafanyabiashara Ifakara mjini – picha na: Isidory Mtunda

Habari hii inaelezea maagizo yaliyotolewa na Jeshi la Polisi wilayani Kilombero kupitia Mkuu wa Usalama Barabarani (DTO) kwa wafanyabiashara wa eneo la barabara ya Kilosa mjini Ifakara, yakiwataka kuachana na tabia ya kuegesha magari ya mizigo ovyo (double parking) ili kuzuia ajali na msongamano. Mkutano huo, uliowaitishwa kwa pamoja na Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) Diventine Nyahoro, ulilenga kujenga ushirikiano wa kiusalama na kibiashara, huku wafanyabiashara wakiwakabili kwa kuahidi kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao.

Na: Isidory Mtunda

Wafanyabiashara wenye maduka na biashara zao pembezoni mwa barabara ya Kilosa mjini Ifakara, wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, wameagizwa kuzingatia sheria za matumizi ya barabara ili kuzuia ajali zinazoweza kuepukika.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Usalama Barabarani Wilaya (DTO) katika mkutano uliowakutanisha wafanyabiashara hao, ulioitishwa kwa pamoja na Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD). Akizungumza kwenye mkutano huo, DTO amesema kuwa kutokana na ufinyu wa barabara hiyo, wafanyabiashara na madereva hawaruhusiwi kuegesha magari ya mizigo huku na huku ovyo (double parking), badala yake wanapaswa kuwa wavumilivu na kusubiriana ili kuepusha usumbufu na hatari kwa watumiaji wengine.

DTO ASP B. Kasongwa akizungumza na wafanyabiashara mjini Ifakara – picha na: Isidory Mtunda
Sauti ya DTO B. Kasongwa

Kabla ya maagizo hayo ya DTO, mkuu wa Polisi wa wilaya (OCD) Diventine Nyahoro alifungua kikao hicho kwa kueleza kuwa lengo kuu la Jeshi la Polisi kuwakutanisha wafanyabiashara hao ni kujenga ushirikiano wa karibu utakaosaidia kutatua changamoto za kiusalama na kibiashara bila kuathiri amani ya mji wa Ifakara.

OCD SP Nyahoro ( wapili kutoka kushoto) – picha na: Isidory Mtunda

Kwa upande wao, wafanyabiashara hao wamepokea maagizo hayo kwa mikono miwili na kuahidi kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao ambao hawakuhudhuria kikao hicho, lengo likiwa ni kushirikiana kulinda usalama na kuzuia ajali zinazoweza kuepukika barabarani.

Sauti za wafanyabiashara