Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
5 June 2026, 14:07
TFS kupitia KNFR kwa kushirikiana na mradi wa FOLUR imetoa mafunzo ya usimamizi shirikishi wa misitu na udhibiti wa moto kwa kamati za maliasili na wajumbe wa serikali kutoka vijiji 11 vya Wilaya ya Mlimba, kwa lengo la kuimarisha uhifadhi wa mazingira.

Na: Isidory Mtunda
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia Hifadhi ya Msitu wa Asili wa Kilombero (KNFR), kwa kushirikiana na mradi wa Food Systems, Land Use and Restoration (FOLUR), umeanza kutoa mafunzo ya usimamizi shirikishi wa misitu na elimu ya udhibiti wa moto kwa kamati za maliasili pamoja na wajumbe wa serikali za vijiji 11 vinavyozunguka hifadhi hiyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, mkoani Morogoro.
Mafunzo hayo yanalenga kuimarisha ushiriki wa jamii katika uhifadhi wa misitu, kuzuia moto na shughuli nyingine zinazoharibu mazingira, pamoja na kuhakikisha usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu.

Akizungumza na Pambazuko FM, mhifadhi kutoka Kituo cha Utafiti wa Bioanuai na Mazingira cha Udzungwa kilichopo Ifakara, Arafat Seif Mtui, amesema mafunzo hayo yatawawezesha washiriki kutambua mbinu bora za kuzuia na kudhibiti moto wa misitu, sambamba na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika kulinda rasilimali za asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo kutoka kijiji cha Idete, akiwemo Rama Mkonongo, Elizabeth Ngela na Salome Kamwembe, wamesema wamepata maarifa muhimu kuhusu njia za kuzuia moto wa misitu na umuhimu wa kushirikisha jamii katika shughuli za uhifadhi. Wameahidi kutumia elimu hiyo kuwafundisha wananchi wenzao ili kuimarisha juhudi za kulinda mazingira katika maeneo yao.

Wakati huo huo, vijiji vilivyoshiriki mafunzo hayo vimeweka maazimio mbalimbali ya kukabiliana na changamoto ya moto wa misitu. Wananchi kutoka kijiji cha Namwawala, akiwemo Sabina Nyoni, Mohamed Ngokwe na Esther Sambakali, wamesema wameazimia kuendelea kutoa elimu kwa jamii, kufanya doria za mara kwa mara, kuboresha sheria ndogo za mazingira na kusafisha njia za kuzuia moto ili kupunguza athari za moto katika hifadhi hiyo.
