Pambazuko FM Radio

Sekiboko aahidi pampu za umwagiliaji Kilombero

2 August 2026, 18:46

Picha ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Husna Sekiboko aliyevaa miwani .( Picha na Henry Mwakifuna )

Pampu hizi zitasaidia kuongeza uzalishaji na kuwawezesha wanakikundi kuimarisha shughuli zao za kilimo pamoja na kurejesha mkopo kwa ufanisi – Husna Sekiboko

Na Henry Mwakifuna

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Husna Sekiboko, ameahidi kutoa pampu mbili za kisasa za umwagiliaji kwa kikundi cha Katindiuka Horticulture kinachonufaika na shughuli za Taasisi ya Enlighten Development Organization (EDO) iliyopo Ifakara, Wilaya ya Kilombero.

Ahadi hiyo ameitoa baada ya kutembelea na kukagua shughuli za kikundi hicho pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili wakulima wadogo.

Mheshimiwa Sekiboko amesema pampu hizo zitaongeza uzalishaji wa mazao kupitia kilimo cha umwagiliaji, kuboresha kipato cha wanakikundi na kukiwezesha kikundi hicho kurejesha mkopo kilionao kwa wakati.

Picha Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Husna Sekiboko, (Picha na Henry Mwakifuna ).

Sauti ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Husna Sekiboko,

Awali, akisoma risala ya kikundi cha Katindiuka Horticulture, Mwenyekiti wa kikundi hicho, Janeth Kongowele, amesema amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana kupitia mafunzo na uwezeshaji walioupata, bado wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vifaa vya kisasa na teknolojia ya kilimo, hali inayopunguza tija na uwezo wa kuongeza uzalishaji.

Janeth amesema changamoto nyingine ni idadi kubwa ya wanawake vijana na akina mama wadogo waliopo katika jamii ambao bado hawajafikiwa na fursa za mafunzo, uwezeshaji na mitaji ya kuanzisha shughuli za kujiongezea kipato.

Ameiomba Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kuendelea kuziunga mkono taasisi kama EDO ili ziweze kuwafikia wanawake wengi zaidi, kuwajengea uwezo na kuwawezesha kujitegemea kiuchumi.

Picha ya Mwenyekiti wa kikundi cha Katindiuka Horticulture, Janeth Kongowele,aliyeshika mic(Picha na Henry Mwakifuna)
Sauti ya Mwenyekiti wa kikundi cha Katindiuka Horticulture, Janeth Kongowele