Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
8 June 2026, 11:48

Viongozi wa kijiji cha Mbingu na kamati ya mazingira wamepatiwa mafunzo ya uhifadhi wa misitu na udhibiti wa moto ili kuimarisha ulinzi wa Msitu wa Asili wa Kilombero na kupunguza uharibifu wa mazingira unaotokana na shughuli za kibinadamu
Na: Isidory Mtunda
Viongozi wa Serikali ya Kijiji cha Mbingu halmashauri ya wilaya ya Mlimba mkoani Morogoro pamoja na wajumbe wa Kamati ya Mazingira wamepatiwa mafunzo ya uhifadhi wa misitu na udhibiti wa moto, yakiwa na lengo la kuimarisha ulinzi wa Msitu wa Asili wa Kilombero (KNFR) dhidi ya uharibifu unaosababishwa na shughuli za uchomaji mkaa, ukataji miti na usafishaji wa mashamba kwa njia ya moto.
Akizungumza na Pambazuko FM, Mtendaji wa Kijiji cha Mbingu, Aziza Makata Masalu, amesema mafunzo hayo yamewaongezea maarifa na mbinu mpya za kuzuia moto wa misitu, ikiwemo kusafisha njia za kuzuia moto, kutoa elimu kwa jamii, kuunda timu za kuzima moto na kufanya doria za mara kwa mara..
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Mazingira katika kijiji hicho, Theresia Mhalami, amesema kamati imekuwa ikifanya doria za mara kwa mara na kuchukua hatua dhidi ya watu wanaojihusisha na ukataji miti, ukusanyaji wa kuni na uchomaji mkaa ndani ya Msitu wa Asili wa Kilombero.
Kwa upande wake, mjumbe wa Kamati ya Mazingira, Veronika John, amesema mafunzo hayo yamemsaidia kupata uelewa zaidi kuhusu mbinu za kuzuia moto wa misitu, ikiwemo kusafisha mipaka na njia za moto kabla ya shughuli za kilimo kuanza.
Mafunzo hayo yametolewa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia Hifadhi ya Msitu wa Asili wa Kilombero (KNFR), kwa kushirikiana na mradi wa Food Systems, Land Use and Restoration (FOLUR), kwa kamati za maliasili na wajumbe wa serikali kutoka vijiji 11 vya Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba kwa lengo la kuimarisha uhifadhi wa mazingira na usimamizi endelevu wa misitu.