Pambazuko FM Radio

Mlimba yalenga kukusanya bilioni 9.3

3 July 2026, 09:49

Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba imepanga kukusanya shilingi bilioni 9.3 kupitia mapato ya ndani katika mwaka wa fedha 2026/2027, ikilenga kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato na kuboresha huduma kwa wananchi.

Na: Kuruthum Mkata

Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba imeweka lengo la kukusanya jumla ya shilingi bilioni 9.3 kupitia vyanzo vya mapato ya ndani katika mwaka wa fedha 2026/2027, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza mapato na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani cha kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (Mkaguzi mkuu wa nje – CEA) wa Mkoa wa Morogoro, kilichofanyika Julai 2, 2026, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, Jamary Idrisa Abdul, amesema halmashauri imejipanga kufikia lengo la kukusanya shilingi bilioni 9.3 kwa kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato kutoka katika vyanzo vyake vyote.

Amesema halmashauri itaendelea kuimarisha usimamizi wa vyanzo vya mapato vilivyopo sambamba na kubuni mikakati mipya ya kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ili kufikia malengo yaliyowekwa.

Sauti ya mkurugenzi wa Mlimba – Jamary Abdul

Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba kwa kuwa kinara wa ukusanyaji wa mapato ya ndani katika Mkoa wa Morogoro.

Malima amesema mafanikio hayo yanapaswa kuwa chachu ya kuongeza juhudi zaidi, akiwataka viongozi na watendaji wa halmashauri hiyo kuendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato kwa weledi, uwazi na uwajibikaji ili Mlimba isiwe kinara wa mkoa pekee, bali iwe mfano wa kuigwa kitaifa.

Sauti ya mkuu wa mkoa wa Morogoro – Adam Malima

Naye Chief External Auditor (CEA) wa Mkoa wa Morogoro, Stephen Kassaro, ameutaka uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba kuhakikisha unatekeleza kwa wakati mapendekezo yote yaliyotolewa katika ripoti ya ukaguzi. Amesema utekelezaji wa mapendekezo hayo utaimarisha usimamizi wa fedha za umma, kuongeza uwajibikaji na kuboresha utendaji wa halmashauri.

Sauti ya Chief External Auditor– C.E.A – Stephen Kassaro

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, Bi. Martha Mkula, ameeleza changamoto ya matumizi ya mfumo wa ujazaji wa lumbesa katika biashara ya mazao, akisema utaratibu huo unasababisha upotevu wa mapato ya halmashauri na kuwaathiri wananchi.

Ametaka hatua stahiki kuchukuliwa ili kudhibiti changamoto hiyo, kuongeza uwazi katika biashara ya mazao na kulinda mapato ya halmashauri kwa manufaa ya maendeleo ya wananchi.

Sauti ya Martha Mkula