Pambazuko FM Radio

Dc Kilombero aagiza changamoto usafi Ifakara kutatuliwa

14 July 2026, 12:53

Wafanyabiashara wa soko kuu Ifakara wakiwa kwenye mkutano na Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Wakili Dunstan Kyobya (Picha na Kuruthumu Mkata)

Soko letu linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uchafu, kukosekana kwa choo bora pamoja na ulinzi hivyo tunaiomba Serikali kupitia Halmashauri ya Mji wa Ifakara itusaidie kutatua changmoto hizi ili tuendelee na biashara zetuWafanyabiashara

Na Kuruthumu Mkata

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara kuhakikisha unatatua haraka changamoto ya usafi katika Soko Kuu la Ifakara ili kuboresha mazingira ya biashara.

Agizo hilo amelitoa leo Julai 14, 2026, wakati wa mkutano wa hadhara kati ya Mkuu huyo wa Wilaya na wafanyabiashara wa soko hilo uliolenga kusikiliza kero zao na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili.

Katika mkutano huo, wafanyabiashara wameeleza changamoto ya hali ya usafi katika soko hilo kuwa ni kero kubwa kwao,Pia wameeleza changamoto nyingine zinazowakabili, zikiwemo upatikanaji wa mikopo, huduma za vyoo pamoja na ulinzi wa mali zao.

Akizungumza katika mkutano huo, Wakili Kyobya amesema suala la usafi linapaswa kupewa kipaumbele, akionya kuwa mazingira machafu yanaweza kusababisha soko kufungwa au kuzuka kwa magonjwa ya mlipuko, ikiwemo kipindupindu.

Picha ya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Wakili Dunstan Kyobya (Picha na Kuruthum Mkata)
Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Wakili Dunstan Kyobya

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Mwalimu Forkwad Mchame, amesema Halmashauri itachukua hatua za kuboresha usafi, kuhakikisha vifaa vinapatikana na kuimarisha ulinzi ndani ya soko hilo. Aidha, amewaomba wafanyabiashara kuwa wavumilivu wakati Halmashauri ikiendelea kuzitatua changamoto hizo.

Picha ya Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Mwalimu Forkwad Mchame, (Picha na Kuruthum Mkata)

Sauti ya Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Mwalimu Forkwad Mchame

Naye Afisa Maendeleo ya Jamii, Mercy Minja, akizungumzia suala la mikopo, amesema changamoto kubwa imekuwa ucheleweshaji wa mchakato wa utoaji wa mikopo Benki kutokana na masharti ya taasisi za kifedha huku Meneja wa Bank ya Nmb akieleza kuwa wafanyabiashara wanaoomba mikopo baadhi hawana vizimba vikubwa vya kufanyia Biashara.

Picha ya Afisa Maendeleo ya Jamii, Mercy Minja (Picha na Kuruthum Mkata)

Sauti ya Afisa Maendeleo ya Jamii, Mercy Minja

Baadhi ya wafanyabiashara wa Soko Kuu la Ifakara akiwemo Thomas Elias wameeleza matumaini yao kuwa serikali itachukua hatua za haraka kutatua changamoto walizowasilisha, hususan usafi wa soko, huduma za vyoo, ulinzi na upatikanaji wa mikopo, ili kuwawezesha kufanya biashara katika mazingira bora na salama.

Picha ya Baadhi ya wafanyabiashara wa Soko Kuu la Ifakara (picha na Kuruthum Mkata)

Sauti za Baadhi ya wafanyabiashara wa Soko Kuu la Ifakara