Pambazuko FM Radio

DC Kilombero aonya waharibifu vyanzo vya maji

5 June 2026, 21:30

Picha ya Mto Lumemo Katika Kijiji cha Kining’ina(Picha na Katalina Liombechi)

Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza umuhimu wa kulinda na kuhifadhi mto Lumemo ambao ni moja ya vyanzo muhimu vya maji vinavyochangia mtiririko wa Mto Kilombero

Na Katalina Liombechi

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili, amesema hatamvumilia mtu yeyote anayejihusisha na shughuli zinazoharibu vyanzo vya maji na mazingira, akieleza kuwa vitendo hivyo vinaweza kukwamisha juhudi za Serikali za kufikia azma ya kuwa na Tanzania ya kijani ifikapo mwaka 2050.

Akizungumza kama mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani leo June 5, 2026 yaliyofanyika katika Kijiji cha Kining’ina, kando ya Mto Lumemo, Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza umuhimu wa kulinda na kuhifadhi mto huo ambao ni moja ya vyanzo muhimu vya maji vinavyochangia mtiririko wa Mto Kilombero.

Picha ya DC Kyobya akizungumza katika maadhimisho siku ya Mazingira Duniani(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya DC Kyobya

Maadhimisho hayo yaliyoongozwa na kaulimbiu ya “Tuwajibike kukijanish Tanzania” katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara yalifanyika kwa ufadhili wa Shirika la Six Rivers Africa kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Halmashauri ya Mji wa Ifakara.

Katika tukio hilo, miti 1,000 ilipandwa katika eneo la Kining’ina kama sehemu ya juhudi za kuimarisha uhifadhi wa mazingira.

Picha ya baadhi ya Watumishi wa Six Rivers Africa,Meneja TFS Kilombero(Picha na Katalina Liombechi)

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Meneja wa Matokeo wa Six Rivers Africa, Marry, amesema shirika hilo linajivunia kuwa sehemu ya wadau wanaoiunga mkono Serikali katika kutekeleza mikakati ya uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji.

Picha ya Mary Marandu Meneja matokeo Six Rivers Africa(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya Marry Marandu Meneja matokeo SRA

Kwa upande wake, Gerald Hamisi, Mtaalamu wa wa maji kutoka Bodi ya Maji Bonde la Rufiji, Kidakio cha Kilombero, amesema taasisi hiyo inaendelea kusimamia na kulinda vyanzo vya maji kupitia utoaji wa elimu kwa jamii pamoja na usimamizi wa sheria zinazohusu matumizi endelevu ya rasilimali za maji.

Sauti ya Gerald Hamisi RUFIJI

Mbali na shughuli za upandaji miti, Six Rivers Africa pia imefadhili mjadala maalum uliohusisha wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Ifakara.

Mjadala huo Umejadili namna teknolojia inavyoweza kutumika kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani mdahalo ambao umekuwa na matokeo chanya kama anavyotueleza Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Mji wa Ifakara Mwalimu Folkward Mchami.

Picha ya Afisa Elimu Halmashauri ya Mji Ifakara(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya Afisa Elimu Sekondari

Baadhi ya wanafunzi walioshiriki mdahalo huo walieleza kufurahishwa na fursa hiyo, wakisema imewapa maarifa mapya na hamasa ya kuwa mabalozi wa utunzaji wa mazingira katika jamii zao.

Nao Wanafunzi hao pia wamelishukuru Shirika la Six Rivers Africa kwa kuandaa mjadala huo pamoja na kutoa zawadi mbalimbali zilizowahamasisha kushiriki kikamilifu katika masuala ya mazingira.

Picha ya Baadhi ya Wanafunzi katika Mdahalo(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti za Wanafunzi

Maadhimisho hayo yameacha ujumbe muhimu kwa jamii juu ya wajibu wa kila mmoja katika kulinda mazingira na vyanzo vya maji kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.