Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
23 April 2026, 19:00

“Utekelezaji wa miradi ya uunganishaji umeme na upanuzi wa vituo vya kupooza umeme inatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya wananchi kwa kuongeza fursa za kiuchumi na kuboresha huduma za kijamii“
Na Katalina Liombechi
Shirika la Umeme Tanzania, TANESCO Mkoa wa Morogoro Kusini linaendelea kutekeleza mikakati ya kuboresha upatikanaji wa umeme, hasa katika maeneo ya vijijini.
Akizungumza na Pambazuko FM, Mhandisi Erick Emanuel Ntiba amesema shirika hilo, kwa kushirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), linaendelea na mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji 68 vya mkoa huo.
Mradi huo unahusisha vitongoji 31 vya Wilaya ya Kilombero ambapo 15 vya Mji wa Ifakara na 16 vya Wilaya ya Mlimba.

Aidha, TANESCO inapanga kuboresha miundombinu ya umeme kwa kupanua kituo cha Kibaoni na kujenga kituo kipya Mahenge ili kuongeza uwezo wa usambazaji.
Wananchi waliopitiwa na miradi hiyo tayari wamelipwa fidia, hatua inayorahisisha utekelezaji wake.
TANESCO pia imetoa wito kwa wananchi kulinda miundombinu ya umeme, ikisisitiza kuwa ni muhimu kwa maendeleo ya taifa.
Kwa ujumla, mikakati hii inaonesha jitihada za TANESCO katika kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na endelevu, jambo ambalo ni msingi muhimu katika kukuza uchumi wa viwanda na kuboresha maisha ya wananchi wa Morogoro Kusini na Tanzania kwa ujumla.