Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
13 May 2026, 19:53

Bodi ya Maji ya Bonde la Rufiji Kidakio cha Kilombero,imekiri kuwepo kwa shughuli zinazotishia mazingira ya vyanzo vya maji
Na Katalina Liombechi
Baadhi ya Vijana na wanawake Kata ya Lumemo katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara wameelezea wasiwasi wao kuhusu hatma ya vyanzo vya maji iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa kuvilinda na kuvitunza.
Wakizungumza na Pambazuko FM kuhusu uelewa wa jamii katika uhifadhi wa vyanzo vya maji, baadhi ya wananchi wa kata hiyo wamebainisha kuwepo kwa shughuli mbalimbali ambazo, kwa mtazamo wao wamesema zinaweza kuhatarisha chanzo cha Mto Lumemo na kusababisha madhara kwa maisha ya binadamu pamoja na viumbe hai kwa ujumla.
Aidha, wamezitaka mamlaka husika kushirikiana kwa karibu na jamii katika kuchukua hatua za haraka na endelevu ili kuokoa vyanzo vya maji.

Kwa upande wake Gerald Hamisi kutoka Bodi ya Maji ya Bonde la Rufiji Kidakio cha Kilombero,amekiri kuwepo kwa shughuli hizo zinazotishia mazingira ya vyanzo vya maji.

Amesema kuwa bodi hiyo, kama msimamizi wa vyanzo vya maji kwa mujibu wa sheria, imekuwa ikiendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kutoa elimu kwa umma kupitia majukwaa tofauti, kushirikiana na jumuiya za watumia maji zilizoanzishwa kisheria, pamoja na kusimamia utekelezaji wa sheria zinazolenga kulinda rasilimali za maji.
