Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
17 May 2026, 11:24

TFS kupitia Hifadhi ya Msitu wa KNFR yapanda miche ya miti takribani 10,000 katika vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo kupitia mradi wa FOLUR, huku wananchi wakieleza manufaa ya msitu katika uhifadhi wa mazingira na uzalishaji wa kilimo.
Na: Isidory Mtunda
Wakala wa huduma za misitu Tanzania kupitia hifadhi ya msitu wa Kilombero Nature Forest Reserve kupitia hifadhi ya msitu wa Kilombero Nature Forest Reserve (KNFR), umefanikiwa kupanda miche ya miti takribani 10,000 katika maeneo ya mipakani mwa hifadhi hiyo kwa kushirikiana na wananchi wa vijiji vinavyoizunguka, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kurejesha mipaka ya hifadhi.

Akizungumza na Pambazuko FM, mhifadhi wa KNFR kanda ya Kilombero Tullah Abong’o, Tullah Abong’o amesema zoezi hilo linalotekelezwa kupitia Mradi wa Urejeshaji wa Mifumo ya Chakula (FOLUR), linalenga kurejesha alama za mipaka katika maeneo ambayo wananchi walikuwa wanashindwa kutambua mipaka halisi ya msitu huo.
Abong’o ameongeza kuwa wananchi kutoka vijiji vya Idete ‘A’, Idete ‘B’, Namwawala, Kisegese, Chiwachiwa, Mpofu, Mbingu, Njage, Mkusi na Mchombe wameendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za upandaji miti na uhifadhi wa mazingira, jambo lililosaidia kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa mradi huo.
Kwa upande wake, katibu wa kamati ya mazingira ya kijiji cha Mpofu, Richard Kidodowaja amesema wananchi wanaozunguka hifadhi ya KNFR wananufaika na uwepo wa msitu huo kutokana na mchango wake katika upatikanaji wa mvua pamoja na kuongeza rutuba ya udongo kupitia majani yanayooza na kutumika kama mbolea ya asili.
