Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
22 June 2026, 20:23

Lengo ni kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia wananchi kwa urahisi zaidi kupitia mawakala wetu waliopo karibu na maeneo
Na Katalina Liombechi
Benki ya CRDB imezindua kampeni ya miezi sita ya “Bonge la Wakala” kupitia huduma ya Simbanking kimpango wako inayolenga kusogeza huduma za kifedha karibu zaidi na wananchi kupitia mtandao wa mawakala waliopo katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza mara baada ya kikao cha kutambulisha na kuzindua kampeni hiyo katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero leo june 22,2026, Meneja Mahusiano wa Huduma za Uwakala Kanda ya Kati Emmanuel amesema kampeni hiyo inalenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za kibenki kwa wateja popote walipo, bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata matawi ya benki.
Ameeleza kuwa kupitia kampeni hiyo, benki inalenga kuhamasisha wananchi kujiunga na mfumo rasmi wa kifedha na kibenki ili waweze kunufaika na huduma mbalimbali zinazotolewa na benki, ikiwemo kuweka na kutoa fedha, kufanya miamala mbalimbali pamoja na kupata fursa za kifedha zinazochochea maendeleo ya kiuchumi.
Ameongeza kuwa kampeni hiyo itafikia makundi mbalimbali ya kijamii yakiwemo wafanyabiashara wadogo na wa kati, wakulima, vijana, wanawake na makundi mengine muhimu katika jamii kwa lengo la kuongeza ushiriki wao katika huduma rasmi za kifedha.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya, ameipongeza benki hiyo kwa hatua yake ya kuendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi.
Amesema juhudi hizo zina mchango mkubwa katika kukuza ujumuishaji wa kifedha na kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi, hususan wa maeneo ya vijijini, katika kupata huduma za kibenki.

Kampeni ya “Bonge la Wakala” inatarajiwa kuendelea kwa kipindi cha miezi sita katika maeneo mbalimbali, huku ikilenga kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za kifedha na kuhamasisha wananchi wengi zaidi kujiunga na mfumo rasmi wa kibenki nchini ambapo kwa mujibu wa Mshawishi wa masuala ya huduma za kibenki kupitia simu wa CRDB amezitaja zawadi mbalimbali zinazotolewa kupitia kampeni hiyo.
Sauti ya Husain CRDB kanda ya kati