Pambazuko FM Radio

Madereva wa Matrekta Mlimba Wapewa Elimu

30 July 2026, 09:47

Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro limefanya mafunzo ya sheria za usalama barabarani kwa wamiliki na madereva wa matrekta na power tiller katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba. Mafunzo hayo yamelenga kupunguza ajali, vifo, na majeraha, huku wataalamu wakifafanua taratibu za usajili wa matela na upatikanaji wa leseni.

Na: Isidory Mtunda

Imeelezwa kuwa kutotii sheria na kanuni za usalama barabarani kunaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo vifo, majeraha, uharibifu wa vyombo vya moto, kurudisha nyuma uchumi, pamoja na kupoteza muda wa uzalishaji kwa kuhudhuria kesi mahakamani.

Hayo yamesemwa na Mrakibu wa Jeshi la Polisi ambaye pia ni Mkuu wa Kituo cha Polisi Mngeta, Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba mkoani Morogoro, Dotto Ngimbwa, wakati wa mafunzo ya sheria za usalama barabarani yaliyowahusisha wamiliki na madereva wa matrekta na power tiller

Sauti ya mkuu wa kituo Mngeta – Ngimbwa

Katika mafunzo hayo yaliyoratibiwa na timu ya usalama barabarani Wilaya ya Kilombero ikiongozwa na ASP Blandina Kasongwa, washiriki waliibua changamoto za upatikanaji wa leseni pamoja na usajili wa matela ya matrekta.

Sauti ya mshiriki Dikson Kiswaga

Akieleza utaratibu wa kusajili matela ya matrekta, ASP Blandina Kasongwa amesema kuwa ili tela liweze kusajiliwa linatakiwa kuwa na mfumo wa umeme, mfumo wa breki, viakisi mwanga (reflectors), pamoja na kuchongewa namba ya chesisi (Chassis number).

Sauti ya ASP Kasongwa

Aidha, ASP Kasongwa amefafanua utaratibu wa kupata mafunzo kwa watakaohitaji, ambapo amewataka wajiorodheshe ili idadi yao ijulikane—ikihusisha wanaohitaji kuhuisha leseni zao pamoja na wale wasiokuwa na leseni kabisa.

Sauti ya ASP Kasongwa

Naye Diwani wa Kata ya Mchombe, Mheshimiwa Batholomeo B. Swala, amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kuamua kutoa elimu kwanza kabla ya kuanza kuchukua hatua za kisheria, huku akiwataka madereva kuacha tabia ya kuendesha vyombo vya moto kwa mwendo kasi.

Sauti ya diwani Swala