Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
17 August 2026, 16:21

Halmashauri ya Mji wa Ifakara wilayani Kilombero inaendelea na mkakati wa kukamilisha maboma ya ofisi za vijiji na kata ambayo bado hayajakamilika. Akijibu swali lililoulizwa na Diwani wa Kata ya Kisawasawa katika Kikao cha Nne cha Baraza la Madiwani, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Rashid Semgoya, amesema kuwa ujenzi na ukamilishaji huo utafanyika hatua kwa hatua kadri ya upatikanaji wa rasilimali na bajeti.
Awali, Diwani wa Kata ya Kisawasawa, Justus Ndege, aliihoji halmashauri hiyo kuhusu kutokamilika kwa boma la ofisi ya kata tangu mwaka 2009, huku akiomba kata hiyo kupewa kipaumbele maalumu kwa kuwa ni miongoni mwa kata kongwe zaidi katika eneo hilo.

Akizungumzia suala la bajeti, Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Ifakara Mji, Kassim Nakapala, amewasihi madiwani wenzake kuzingatia na kusimamia kwa uaminifu mipango yote iliyopitishwa kwenye bajeti ya halmashauri ili kuchochea maendeleo.

Katika hatua nyingine, kikao hicho kilipata fursa ya kuipongeza halmashauri hiyo kwa kufanya vizuri na kuibuka washindi wa nafasi ya pili katika Maonesho ya Wakulima (Nane Nane) ya mwaka 2026 kwa Kanda ya Mashariki.