Pambazuko FM Radio

Wazee wataka uwakilishi vyombo vya maamuzi

11 September 2026, 13:12

wazee walioshiriki siku ya wazee ki-mkoa kata ya Mwaya – picha na: Daudi Moses Mbanile

Baraza la ushauri la wazee mkoa wa Morogoro limeitaka serikali na halmashauri kuongeza ushirikishwaji wa wazee katika vyombo vya maamuzi, likisema ushiriki wao bado haujawa wa kutosha. Serikali kwa upande wake imeahidi kuhakikisha wazee wanapata uwakilishi katika vikao vya maamuzi kuanzia ngazi ya kijiji na mtaa hadi mkoa, huku ikieleza kuwa Mkoa unakabiliwa na upungufu wa Maafisa Ustawi wa Jamii.

Na; Isidory Mtunda

Baraza la ushauri la wazee mkoa wa Morogoro limeitaka serikali na halmashauri kuongeza ushirikishwaji wa wazee katika vyombo vya maamuzi, likisema kundi hilo lina uzoefu na mchango muhimu katika maendeleo ya jamii.

Baraza hilo limesema ushiriki wa wazee katika vikao vya maamuzi bado haujawa wa kutosha, licha ya kuwepo kwa mabaraza ya wazee kuanzia ngazi ya vijiji na mitaa hadi taifa, amesema Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la wazee mkoa wa Morogoro, mzee Samweli Mpeka.

Samweli Mpeka – M/kiti baraza la wazee Morogoro – picha na: Daudi Moses Mbanile
sauti ya Samweli Mpeka

Ikijibu maombi hayo, Serikali imeeleza kuwa wazee wanapaswa kuwa na wawakilishi katika vikao mbalimbali vya maamuzi kuanzia ngazi ya kijiji, mtaa, kata, wilaya hadi mkoa.

Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya ya Kilombero, wakili Dunstan Kyobya, aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Morogoro, Mhe. Queen Cuthbert Sendiga

Mkuu wa wilaya wakili Dunstan Kyobya – picha na: Daudi Moses Mbanile
sauti ya DC Dunstan Kyobya

Wakati huo huo, mkuu huyo wa wilaya amesema mkoa unatambua changamoto ya upungufu wa Maafisa Ustawi wa Jamii, ambapo kwa sasa wapo watumishi 85 sawa na asilimia 26 ya mahitaji ya watumishi 329, na kwamba hatua zimeanza kuchukuliwa ili kuimarisha upatikanaji wa watumishi hao.