Pambazuko FM Radio

Milioni 789 kuleta neema Ifakara Mji

23 September 2026, 18:32

mikopo hiyo inalenga kuwawezesha wananchi kujiongezea kipato na kuimarisha shughuli za kiuchumi- Bi. Pili Kitwana-mkurugenzi mji ifakara.

Wakili Dunstan Kyobya Mkuu wa Wilaya Kilombero, Bi Pili Kitwana Mkurugenzi Ifakara Mji wakiwa na Baadhi ya Wanufaika wa Mikopo ya Asilimia Kumi Picha na Eliasi Maganga

Na Elias Maganga

Halmashauri ya Mji wa Ifakara imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 789.2 kwa vikundi 84 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika mwaka wa fedha 2025/2026. Fedha hizo zimetokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri.

Bi Pili Kitwana, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ifakara Mji picha na Elias Maganga

sauti ya Mkurugenzi Bi Pili Kitwana

Akizungumza katika hafla ya utoaji wa mikopo iliyofanyika katika viwanja vya Soko Kuu la Ifakara, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Bi. Pili Kitwana, amesema mikopo hiyo inalenga kuwawezesha wananchi kujiongezea kipato na kuimarisha shughuli za kiuchumi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Kassim Nakapala, amevitaka vikundi vilivyonufaika kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kutoa nafasi kwa vikundi vingine kunufaika. Amesisitiza kuwa halmashauri haitamvumilia mtu au kikundi kitakachoshindwa kurejesha fedha hizo bila sababu za msingi.

sauti ya Mwenyekiti wa Ifakara Mji

Wakili Dunstan Kyobya, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero picha na Elias Mganga

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, amewataka wanufaika kutumia fedha hizo kwa shughuli zilizokusudiwa na kuepuka matumizi yasiyo na tija. Pia amewaagiza maafisa maendeleo wa kata kufuatilia utekelezaji wa miradi inayotekelezwa kwa mikopo hiyo na kuendelea kutoa elimu kwa vikundi ambavyo bado havijasajiliwa ili vipate fursa ya kunufaika.

sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero

Baadhi ya Wanufaika wa Mikopo ya Asilimia 10 kutoka Mji wa Ifakara picha na Elias Maganga

Baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo wameishukuru Halmashauri ya Mji wa Ifakara kwa kuwawezesha kupata mtaji unaowasaidia kuboresha maisha yao. Wamesema watahakikisha wanarejesha mikopo kwa wakati ili kuendelea kujenga uaminifu na kuwezesha vikundi vingine kupata fursa hiyo.

sauti ya Baadhi ya Wanufaika