Pambazuko FM Radio

Wazawa kunufaika na Ajira za Mradi wa Maji wa Bilioni 48 Ifakara

5 October 2026, 14:13

Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuzalisha ajira kupitia miradi ya maendeleo, hivyo vijana wa maeneo husika wanapaswa kupewa kipaumbele katika nafasi zinazojitokeza-Naibu Waziri Maji

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Andrew Mathew akikagua mradi wa Maji Kiburubutu, Ifakara Wilayani Kilombero picha na Kuruthum Mkata

Na Kuruthum Mkata

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Andrew Mathew, ameitaka jamii inayozunguka Mradi wa Maji wa Kiburubutu mjini Ifakara kuhakikisha inanufaika na fursa za ajira zinazotokana na utekelezaji wa mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 48.

Mhandisi Mathew ametoa kauli hiyo wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo uliopo Kata ya Kibaoni, Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Wilaya ya Kilombero Ambapo Amesema Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuzalisha ajira kupitia miradi ya maendeleo, hivyo vijana wa maeneo husika wanapaswa kupewa kipaumbele katika nafasi zinazojitokeza.

Baadhi ya Viongozi na Wahandisi walioongozana na Naibu Waziri wa Maji wakiwa katika Eneo la Mradi wa maji Kiburubutu picha na Kuruthum Mkata

Aidha, amewataka wakandarasi wanaotekeleza mradi huo kuhakikisha wanaacha alama chanya kwa jamii kwa kushiriki ujenzi wa miundombinu ya kijamii ikiwemo zahanati, shule na huduma nyingine muhimu.

sauti ya Naibu Waziri wa Maji

Sehemu ya Wahandisi wakiwa katika mradi wa maji Kiburubutu Ifakara Picha na Kuruthum Mkata

Kwa upande wake, Meneja wa IFAUWASA, Mhandisi Hamad Mpambaike, amesema mkandarasi ameongezewa muda wa utekelezaji na kwamba mradi unatarajiwa kukamilika Novemba 22 mwaka huu. Amesema hadi sasa utekelezaji umefikia asilimia 71.5.

sauti ya Meneja wa Maji Ifakara

Naye Mbunge wa Jimbo la Kilombero, Abubakary Asenga, amesema changamoto kubwa ya maji katika jimbo hilo imepungua kutokana na utekelezaji wa Mradi wa Kiburubutu, huku akibainisha kuwa Kata ya Mang’ula bado inakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa chanzo cha maji.

sauti ya Mbunge wa Kilombero Abubakari Assenga

Akizungumza kwa niaba ya wenyeviti wa mitaa ya Ifakara, Mwenyekiti wa Mtaa wa Upogolo amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mradi huo, akisema wananchi wanahitaji kuona matokeo ya miradi ya maendeleo katika maisha yao ya kila siku.

sauti ya Mwenyekiti wa Mtaa wa Upogolo Halmashauri ya Mji wa Ifakara

Mradi wa Maji wa Kiburubutu unatarajiwa kuhudumia mitaa 28 ya Mji wa Ifakara na kunufaisha wakazi zaidi ya 80,000 mara utakapokamilika Novemba 22, 2026.