Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
28 November 2026, 09:17

Fursa hiyo inaleta manufaa ya kiuchumi na kutunza mazingira na kwamba serikali na wadau wapo tayari kutoa ushirikiano kwa wanaotaka kuifanyia kazi
Na Katalina Liombechi
Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (IUCN) limehimiza matumizi ya makapi na mabua ya mpunga katika uzalishaji wa bidhaa mbadala, ikiwemo mkaa mbadala na chakula cha mifugo, ili kuongeza fursa za kiuchumi kwa jamii na kuimarisha uhifadhi wa mazingira.
Wito huo umetolewa katika kikao kazi kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, mjini Ifakara, kilichojadili fursa na mzunguko wa biashara kupitia mpango wa matumizi ya mabaki ya zao la mpunga kama malighafi ya bidhaa mbalimbali zenye thamani ya kiuchumi.
Afisa Mazingira Halmashauri ya Mji wa Ifakara Salome Mayenga na Mchumi Kilimo Alexander Mpwaga ambaye alikuwa mwezeshaji katika kikao hicho wamesema watakaoikimbilia fursa hiyo watapata manufaa ya kiuchumi huku wakitunza mazingira na kwamba wapo tayari kutoa ushirikiano kwa wanaotaka kuifanyia kazi.

Baadhi ya walioshiriki kikao hicho Diana Mbuba kutoka Taasisi ya Mazingira ni Uhai pamoja na wanaojihusisha na utengenezaji na matumizi ya mkaa mbadala Restituta Luanda kutoka MACCO Mang’
ula licha ya kulishukuru shirika IUCN kwa kuandaa kikao hicho wameelezea uzoefu wao katika fursa ya mkaa mbadala na kuwahiumiza zaidi vijana kuona fursa hii ili kujiingizia kipato na kuwa sehemu ya utunzaji wa mazingira.
Akielezea historia ya Miradi waliyoitekeleza Samuel Kajiba Afisa Miradi kutoka IUCN amesema Kikao hicho kinafanyika wakati IUCN ikielekea kuhitimisha miradi pacha ya SUSTAIN PRO na SUSTAIN ECO iliyotekelezwa kwa kipindi cha miaka minne tangu mwaka 2022, na kuacha matokeo katika mnyororo wa thamani wa zao la mpunga kupitia kilimo shadidi, uhifadhi wa vyanzo vya maji, udhibiti wa taka hatarishi na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Miradi hiyo pia imechangia kuimarisha dhana ya Afya Moja, uhifadhi wa bioanuwai, ustahimilivu wa jamii dhidi ya mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika shughuli za uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya kiuchumi kwa kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali.

Mradi wa SUSTAIN PRO, uliofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Norway, ulijikita katika kuboresha mifumo ya uzalishaji wa chakula, huku SUSTAIN ECO, uliofadhiliwa na Serikali ya Sweden, ukilenga kuimarisha usimamizi endelevu wa mazingira.