Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
27 November 2026, 17:49

DC Kyobya amewataka wahitimu Mafunzo ya Jeshi la akiba kuzingatia misingi ya uadilifu, weledi, nidhamu na haki wanapotekeleza majukumu yao
Na Kuruthumu Mkata
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, amefunga mafunzo ya Jeshi la Akiba yaliyohusisha vijana zaidi ya 100 katika viwanja vya Shule ya Msingi Kisawasawa, wilayani Kilombero.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kyobya amewataka wahitimu hao kuzingatia misingi ya uadilifu, weledi, nidhamu na haki wanapotekeleza majukumu yao katika jamii ambapo pia amewataka watendaji wa kata kuhakikisha vijana hao wanapewa kipaumbele katika fursa za ajira zinapojitokeza katika maeneo yao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi cha JKT, Luteni Kanali Ashrafu Hassan, amewataka wahitimu kufanya kazi kwa bidii, haki na bila kuwaonea wananchi, akisisitiza kuwa wananchi ndio wanaopaswa kuwatumikia.

Naye Kamishna Mwandamizi wa Polisi (SACP), Zarau Mpangule, amesema kiapo walichokula kinapaswa kuwa msingi wa kuwatumikia na kuwalinda wananchi badala ya kutumia nguvu vibaya au kuwanyanyasa.
Baadhi ya wahitimu, akiwemo Said Said, wameishukuru Serikali kwa kuwapatia mafunzo hayo, wakieleza kuwa wamejifunza mambo mbalimbali ikiwemo nidhamu, huku wakieleza pia changamoto walizokutana nazo wakati wa mafunzo.