Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
15 October 2026, 10:30

Hatua za kutatua changamoto zilizopo zimeanza kuchukuliwa, ambapo takribani asilimia 60 ya changamoto hizo zimeanza kushughulikiwa–Mwalimu Mpako.
Na Henry Mwakifuna
Uhaba wa walimu wenye utaalamu, miundombinu isiyokuwa rafiki na upungufu wa vifaa vya kufundishia ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara.
Akizungumza katika mahojiano na Pambazuko FM, Afisa Elimu Maalum wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Mwalimu Abdallah Mpako, ametaja pia idadi kubwa ya wanafunzi darasani, unyanyapaa katika jamii pamoja na ufinyu wa bajeti na ufadhili kuwa miongoni mwa changamoto zinazoathiri utoaji wa elimu kwa wanafunzi hao.
Mwalimu Mpako ameeleza kuwa uhaba wa walimu wenye ujuzi na utaalamu maalum, pamoja na zana za kufundishia na kujifunzia, unaonesha umuhimu wa kuongeza rasilimali zinazolenga mahitaji ya wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Aidha, unyanyapaa na mitazamo hasi dhidi ya watu wenye mahitaji maalum katika jamii ni changamoto inayoweza kujitokeza pia shuleni, hali inayoweza kuathiri ushiriki na ustawi wa wanafunzi hao.
Ameeleza umuhimu wa kutenga bajeti maalum kwa ajili ya elimu ya wanafunzi wenye mahitaji maalum ili kuboresha upatikanaji wa walimu wenye utaalamu, vifaa saidizi na miundombinu rafiki.