Pambazuko FM Radio

Uhifadhi endelevu kuwanufaisha vijiji 15 Bonde la Kilombero

22 October 2026, 14:37

sehemu ya eneo la Bonde la Mto Kilombero picha na Mtandao

Kuhifadhi kutatupelekea kusaidia kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia nchi na kipato kinapatikana kutokana na Biashara ya Hewa Ukaa-Katibu Msaidizi ILUMA.

Na Henry Mwakifuna

Uhifadhi endelevu katika Eneo la Usimamizi wa Wanyamapori la Ifakara, Lupiro na Mangula (ILUMA) umeendelea kuwanufaisha wananchi wa vijiji 15 vilivyopo katika Bonde la Kilombero kupitia mapato yanayotokana na shughuli za uhifadhi.

Katibu Msaidizi wa ILUMA, Issaya Emmanuel Maduhu, amesema uhifadhi ni muhimu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, huku ukichangia kuboresha maisha ya wananchi wanaozunguka eneo hilo.

Amesema vijiji vinavyounda ILUMA vinanufaika na mapato yatokanayo na gawio la uwindaji wa kitalii pamoja na michango ya taasisi mbalimbali zinazotekeleza shughuli zake ndani ya eneo hilo.

Maduhu ameongeza kuwa mapato hayo yanaelekezwa katika miradi ya maendeleo ya kijamii, ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa shule, zahanati na huduma nyingine muhimu kwa wananchi.

Eneo la ILUMA linajumuisha maeneo ya vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Nyerere katika Tarafa za Ifakara na Mangula, wilayani Kilombero, pamoja na Tarafa ya Lupiro, wilayani Ulanga.