Pambazuko FM Radio

Wakulima Bonde la Kilombero wahamasishwa kutumia Mbegu Bora

16 November 2026, 14:47

Wadau wa Uzalishaji Mbegu Kongani ya Mlimba ya Mradi wa Kilimo Jumuishi cha Mnyororo wa Mpunga (IRVC) wakizungumza na Pambazuko FM Picha na Henry Mwakifuna

matumizi ya mbegu kwa mazoea bila kuzingatia ubora wake yanaweza kuathiri uzalishaji, hivyo wakulima wanapaswa kufanya maamuzi sahihi kuhusu aina ya mbegu wanazotumia ili kupata mavuno yenye tija na kukuza kilimo cha kibiashara–Bibi Shamba

Na Henry Mwakifuna

Wakulima wa Bonde la Kilombero wametakiwa kuachana na kilimo cha mazoea na badala yake kutumia mbegu bora pamoja na kuzingatia kanuni za kilimo ili kuongeza uzalishaji, ubora wa mazao na tija katika shughuli zao za kilimo.

Wito huo umetolewa na Denisia Samuel, Bibi Shamba wa Mradi wa Kilimo Jumuishi cha Mnyororo wa Mpunga (IRVC), unaofadhiriwa na Shirika la Norges Vel na kutekelezwa na shirika la Nafaka Kilimo wakati akizungumza na Pambazuko FM, ambapo amesisitiza umuhimu wa wakulima kujitambua na kuthamini shughuli wanazozifanya kwa kuwekeza katika mbinu bora za kilimo na kulenga soko

Denisia Samuel( Kushoto) Bibi Shamba wa Mradi wa IRVC akizungumza na Wakulima kupitia Redio Pambazuko FM Picha na Henry Mwakifuna

sauti ya Bibi Shamba

Kwa upande wao, wadau wa Kongani za Kilimo za Mlimba na Malinyi, Marcela Chipindi, Aurelian Chuma, Steven Msafiri na Justine Ndege, wamewataka wakulima kuzingatia tofauti kati ya nafaka kwa ajili ya chakula na mbegu kwa ajili ya kupanda.

Wamesisitiza kuwa wakulima wanapaswa kuacha tabia ya kutumia nafaka zilizotengwa kwa matumizi ya chakula kama mbegu, wakieleza kuwa chakula ni chakula na mbegu ni mbegu, hivyo matumizi ya mbegu bora ni hatua muhimu katika kuboresha uzalishaji wa mpunga.

Kwa ujumla, wakulima wametakiwa kubadilika kutoka kilimo cha mazoea na kukifanya kilimo kuwa shughuli ya kibiashara inayozingatia ubora wa pembejeo, kanuni za kilimo na tija.

Wadau wa Mradi wa Kilimo Jumuishi cha Mnyororo wa Mpunga (IRVC) Kongani ya Malinyi wakizungumza na Pambazuko FM picha na Hemry Mwakifuna