Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
7 October 2026, 15:40
“Mwanafunzi anatakiwa kuwa amesajiliwa rasmi chuoni, akamilishe taratibu za NIDA na Learner Licence, afaulu mitihani ya ndani kwa kiwango kinachotakiwa, na kufuata hatua zote zinazohusiana na mifumo ya taasisi husika,” amesema Mwambene.

Sehemu ya Ndani ya Gari picha na Henry Mwakifuna
Na Henry Mwakifuna
Wanafunzi wanaojiunga na mafunzo ya udereva katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Ifakara (FDC) wametakiwa kuzingatia taratibu mpya za usajili na upatikanaji wa Leseni ya Udereva, ambazo zinahusisha usajili wa taarifa za mwanafunzi katika mifumo mbalimbali.
Akizungumza na Pambazuko FM kuhusu taratibu hizo, Mratibu wa Mafunzo na Usajili wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Ifakara, Asukile Mwambene, amesema mwanafunzi anapaswa kuanza kwa kuhakikisha amekamilisha usajili wa NIDA, kabla ya kuendelea na hatua nyingine za mchakato wa mafunzo ya udereva.

Mratibu wa Mafunzo na Usajili wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Ifakara, Asukile Mwambene muda mfupi baada ya Mahojiano na Pambazuko FM Picha na Henry Mwakifuna
Amesema baada ya kukamilisha usajili unaohitajika, mwanafunzi anatakiwa kukata Learner Licence na kuendelea na mafunzo pamoja na mitihani ya ndani ya chuo.
Kwa mujibu wa Mwambene, mwanafunzi anatakiwa kupata alama zisizopungua 70 katika mitihani ya ndani ili kufikia kiwango kinachohitajika cha ufaulu.
Ameeleza kuwa mchakato wa mafunzo na upatikanaji wa vyeti na Leseni ya Udereva unahusisha mifumo ya taasisi tatu, ambayo ni Chuo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Jeshi la Polisi.
Mwambene amesema mfumo wa chuo unahusika katika kuhakikisha mwanafunzi amesajiliwa rasmi na amepitia mafunzo, huku TRA ikihusika na taratibu za Leseni ya Udereva, pamoja na hatua nyingine zinazohitajika katika mfumo.
Aidha, amesema Jeshi la Polisi linahusika katika hatua za uhakiki na mchakato unaohakikisha mwanafunzi aliyekidhi vigezo anafanikiwa kupata Leseni ya Udereva kwa kufuata taratibu zilizowekwa.
Amesisitiza kuwa wanafunzi wanapaswa kuhakikisha taarifa zao za usajili zinaendana katika mifumo husika na kukamilisha kila hatua kwa usahihi ili kuepuka changamoto au ucheleweshaji katika mchakato wa kupata Leseni ya Udereva.
sauti ya Asukile Mwambene
Taratibu hizo zinalenga kuweka utaratibu unaoeleweka katika usajili, mafunzo, tathmini na mchakato wa mwanafunzi kufikia hatua ya kupata Leseni ya Udereva.