Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
25 November 2026, 21:11

Wakulima wanaolima katika maeneo ya Ulanga na Mlimba, hulazimika kulipa ushuru wanaporudisha mazao yao, hata wanapokuwa na gunia moja
Na Katalina Liombechi
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kupitia upya utaratibu wa ukusanyaji wa ushuru wa mazao katika geti la Kivukoni–Ulanga na Idete–Mlimba, ili kutekeleza maelekezo ya Rais ya kutowatoza ushuru wakulima wenye mazao yasiyozidi tani moja.
Agizo hilo amelitoa leo Novemba 25, 2026,Akiwa Ifakara kufuatia Mbunge wa Jimbo la Kilombero, Abubakar Asenga, kuwasilisha kero ya wakulima wanaolima katika maeneo ya Ulanga na Mlimba, ambao hulazimika kulipa ushuru wanaporudisha mazao yao, hata wanapokuwa na gunia moja.
Akizungumza mbele ya Waziri Mkuu, Asenga amesema baadhi ya wakulima wamekuwa wakitozwa zaidi ya shilingi 5,000 kwa gunia moja, hali inayowaongezea mzigo wa gharama na kuathiri kipato chao.
Ameeleza kuwa aliwahi kuwasilisha malalamiko hayo mwaka 2024 wakati Rais alipotembelea Ifakara.

Akijibu hoja hiyo, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mh.Queen Sendiga kuhakikisha utaratibu huo unafanyiwa mapitio na maelekezo ya Rais yanazingatiwa katika ukusanyaji wa ushuru wa mazao.
Amesema pamoja na Halmashauri kuwa na wajibu wa kukusanya mapato kwa ajili ya kujiendesha, ukusanyaji huo unapaswa kuzingatia uhalisia na kuepuka kuwaumiza wananchi.

Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba leo baada ya kuzungumza na wananchi Wilayani Kilombero atahitimisha ziara yake kesho Novemba 26,2026 katika Wilaya za Mvomero na Manispaa ya Morogoro hivyo kutimiza siku 5 za ziara yake mkoani Morogoro tangu alipoianza Novemba 21,2026.