Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
10 August 2026, 12:45

Jeshi la Polisi Wilaya ya Kilombero limewataka madereva wa bodaboda, bajaji na guta kuzingatia sheria za usalama barabarani, ikiwemo kutobeba abiria zaidi ya mmoja kwa bodaboda na bajaji, huku guta likisisitizwa kuwa chombo cha kubeba mizigo.
Na; Kuruthum Mkata
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kilombero (OCD), SP Diventine Nyahoro, amepiga marufuku matumizi ya vyombo vya moto, ikiwemo bodaboda na bajaji, kubeba abiria zaidi ya mmoja, huku akisisitiza kuwa guta ni chombo cha kubeba mizigo na si abiria.

Akizungumza wakati wa kufungua kikao cha madereva wa bajaji, bodaboda na guta wilayani Kilombero, OCD SP Nyahoro amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha usalama wa watumiaji wa barabara. Amewataka wamiliki wa vyombo hivyo kuhakikisha madereva wanaowaajiri wanazingatia sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Usalama Barabarani Wilaya ya Kilombero, DTO ASP Blandina Kasongwa, amewataka madereva kuhakikisha vyombo wanavyoviendesha vimesajiliwa na vina nyaraka halali, huku madereva wakiwa na leseni zinazotambulika kisheria. Amesisitiza kuwa uzingatiaji wa sheria za usalama barabarani ni muhimu katika kupunguza ajali.

Naye Ofisa Mfawidhi wa LATRA Ifakara, Amani Mwakalebela, amesema viwango vipya vya tozo vilianza kutumika Julai mwaka huu, ambapo tozo kwa bodaboda imeongezeka kutoka shilingi 17,000 hadi 22,000, huku bajaji ikiongezeka kutoka shilingi 22,000 hadi 32,000.
