Pambazuko FM Radio

Vijana 50 wapatiwa mafunzo mbasa

23 June 2026, 07:09

Vijana 50 wa Kata ya Mbasa, Halmashauri ya Mji Ifakara, wamepatiwa mafunzo ya ujasiriamali, afya ya uzazi na stadi za maisha na Shirika la WISE, yakilenga kuwawezesha kujiajiri na kuboresha maisha yao kiuchumi.

Na: Isidory Mtunda

Vijana wapatao 50 kutoka Kata ya Mbasa, Halmashauri ya Mji Ifakara mkoani Morogoro, wamepatiwa mafunzo ya ujasiriamali, afya ya uzazi na stadi za maisha yaliyoandaliwa na Shirika lisilo la kiserikali la WISE kupitia mradi wa kuwawezesha vijana kiuchumi.

Akizungumza na Pambazuko FM baada ya mafunzo hayo, Mratibu wa Mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi kutoka WISE, Fidelis Yunde, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea vijana uwezo wa kujitegemea kiuchumi na kuboresha maisha yao pamoja na familia zao.

Sauti ya bwana Yunde

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, akiwemo Asha Said, Biliuda Chahowa na Sofia Matola, wamesema changamoto zinazowakabili katika shughuli za kilimo ni pamoja na ukosefu wa maeneo ya kulima, mbegu bora na pembejeo za kilimo. Wameiomba WISE kuendelea kuwasaidia kupata suluhisho la changamoto hizo.

Sauti za washiriki wa mafunzo

Akijibu hoja hizo, Yunde amesema tayari vijana hao wameunganishwa na taasisi mbalimbali zitakazowasaidia kupata pembejeo na huduma muhimu za kilimo, huku akiwahamasisha vijana wengine kutumia fursa zinazotolewa kupitia mradi huo.

Sauti ya bwana Yunde 2

Naye Afisa Kilimo wa Kata ya Mbasa, Eva Privatus, amesema mafunzo hayo yameonesha kuwa vijana wengi wana hamasa ya kuingia katika shughuli za uzalishaji mali, ambapo zaidi ya asilimia 60 wameonesha nia ya kujihusisha na kilimo, huku wengine wakivutiwa na biashara na ushonaji.

Sauti ya afisa kilimo Eva Privatus

Kwa upande wake, Afisa Kilimo kutoka Shirika la East-West Seed, Winnie Kessy, ameahidi kuendelea kuwapatia vijana hao ushauri na msaada wa kitaalamu katika hatua ya utekelezaji wa shughuli zao za kiuchumi.

Sauti ya afisa kilimo Winnie Kessy

Akifunga mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Maendeleo, Omary Sambula, amewataka vijana kutumia maarifa waliyoyapata kujikwamua kiuchumi, kujenga maisha bora na kuepuka utegemezi katika jamii.

Sauti ya bwana Sambula