Pambazuko FM Radio

Polisi wasisitiza usalama wa Matrekta

31 July 2026, 15:17

wamiliki na madeeva wa Matrekta na Power tiller wakimsikiliza DTO Blandina Kasongwa Picha na:WP9079 Mary Bayo

Polisi wa Usalama Barabarani wamewapa elimu wamiliki na madereva wa matrekta na power tiller katika Kata ya Chita, huku wakisisitiza marekebisho ya vyombo hivyo na ufuataji wa taratibu za usajili na leseni ili kupunguza ajali.

Na: Isidory Mtunda

Wamiliki na madereva wa matrekta na power tiller katika Kata ya Chita, Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba mkoani Morogoro, wameiomba Timu ya Usalama Barabarani kuwapa muda wa kurekebisha dosari zilizopo kwenye vyombo vyao ili kupunguza ajali zinazochangiwa na matumizi ya vyombo hivyo.

baadhi ya washiriki wa mafunzo kwa wamiliki na madereva wa Matrekta & Power tiler – Picha na:WP9079 Mary Bayo

Maombi hayo yametolewa wakati wa mafunzo ya usalama barabarani yaliyotolewa na Timu ya Usalama Barabarani iliyoongozwa na ASP Blandina Kasongwa, yenye lengo la kuwajengea uelewa wamiliki na madereva kuhusu matumizi salama ya matrekta na power tiller.

Akizungumzia suala la usajili wa matela ya trekta, ASP Blandina Kasongwa amesema matela mengi hayajakidhi vigezo vinavyotakiwa. Kutokana na hali hiyo, amepiga marufuku matrekta yenye matela yasiyokidhi masharti kufanya shughuli za usiku hadi yatakapofanyiwa marekebisho. Pia amewataka wahusika kuanza mara moja kufanya maboresho yanayowezekana.

ASP Blandina Kasongwa – Picha na:WP9079 Mary Bayo

Kwa upande wake, Mkaguzi wa Magari wa Wilaya ya Kilombero, Sajenti Rajabu Kadikarange, amefafanua kuhusu utaratibu wa upatikanaji wa leseni za udereva. Amesema madaraja ya leseni kama E na C yanapatikana baada ya dereva kuwa na uzoefu wa angalau miaka mitatu, hivyo haiwezekani kuruka kutoka daraja la awali na kwenda moja kwa moja kusomea madaraja hayo.

Mkaguzi wa magari Kilombero SGT Kadikarange – Picha na:WP9079 Mary Bayo
Sauti ya mkaguzi wa magari SGT Kadikarange

Akihitimisha mafunzo hayo, ASP Blandina Kasongwa amewaagiza wamiliki na madereva wote kujiorodhesha ili idadi yao itambuliwe kwa urahisi. Aidha, amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi halipokei fedha za mafunzo wala ada za leseni, na kwamba malipo yote yanapaswa kufanyika kupitia Control Number zilizotolewa na mamlaka husika.

Sauti ya ASP Kasongwa