Pambazuko FM Radio

Lasting Forest yatoa mafunzo hewa ukaa Kilombero

6 June 2026, 09:20

Picha ya Wataalam wa Lasting Forest Solutions na wanufaika wa mafunzo(Picha na Kuruthumu Mkata)

Biashara ya hewa ukaa itasaidia kupunguza hewa chafu inayoweza kuathiri afya za wananchi pamoja na kuchangia ongezeko la mapato kwa jamii

Na Kuruthumu Mkata

Kampuni ya Lasting Forest Solutions imetoa mafunzo ya elimu kuhusu hewa ukaa na ushoroba kwa wajumbe wa Kamati Tendaji ya Pamoja ya Udzungwa–Nyerere (JMC), kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu usimamizi wa miradi ya mazingira na manufaa yake kwa jamii.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Joseph Mwalugelo amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa yataisaidia kamati kutambua wajibu wake, hususan katika masuala ya kisheria, ufuatiliaji wa miradi na kuwahudumia wananchi katika maeneo yanayonufaika na mpango wa hewa ukaa.

Ameeleza kuwa mradi wa hewa ukaa umeanza kuleta manufaa kwa wananchi, ambapo vijiji vilivyopo katika Kata ya Mangula tayari vimepata gawio la shilingi milioni kumi kila kijiji kutokana na mapato ya mradi huo.

Picha ya Joseph Mwalugelo(Picha na Kuruthumu Mkata)
Sauti ya Joseph Mwalugelo Kaimu 1

Mwalugelo pia amebainisha kuwa mradi wa hewa ukaa una faida mbalimbali ikiwemo kupunguza hewa chafu inayoweza kuathiri afya za wananchi pamoja na kuchangia ongezeko la mapato kwa jamii kupitia fedha zinazotokana na biashara ya hewa ukaa.

Sauti ya Joseph Mwalugelo Kaimu 2

Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo ambao ni wenyeviti wa vijiji kutoka Kata ya Mangula, wameishukuru kampuni ya Lasting Forest Solutions kwa kuwapatia elimu hiyo muhimu.

Wamesema maarifa waliyoyapata yatawasaidia kutoa elimu kwa wananchi katika maeneo yao ili kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira na kunufaika na fursa zinazotokana na miradi ya hewa ukaa.

Picha ya Wanufaika wakipatiwa mafunzo ya Hewa ukaa(Picha na Kuruthumu)
Sauti za wenyeviti wanufaika wa mafunzo