Pambazuko FM Radio

STEP yakuza ufugaji bora kuku wa kienyeji Ifakara

29 May 2026, 10:44

Picha ya Washiriki wa Mafunzo ya ufugaji na afya ya kuku Kikundi cha Tunza Mazingira Lumemo (Picha na Katalina Liombechi)

STEP kupitia ufadhili wa Polish aid wanalenga kuendeleza ufugaji bora wa kuku wa kienyeji kama njia muhimu ya kuongeza kipato cha familia na jamii

Na Katalina Liombechi

Shirika linalojihusisha na uhifadhi wa tembo kusini mwa Tanzania,Southern Tanzania Elephant Program (STEP) kupitia ufadhili wa Polish Aid, limeendelea kuvijengea uwezo vikundi mbalimbali katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara kwa kutoa mafunzo ya ufugaji kuku wa kienyeji.

Mafunzo hayo yamejikita katika afya ya kuku pamoja na namna ya kukabiliana na magonjwa yanayoathiri mifugo hiyo.

Akizungumza Mei 28, 2026 katika Kata ya Lumemo, Mratibu wa Mahusiano na maisha endelevu kutoka STEP, Catherine Kimario, amesema mafunzo hayo yameandaliwa baada ya kubaini kuwa ufugaji wa kuku wa kienyeji una mchango mkubwa katika kuongeza kipato kwa wananchi.

Amesema elimu hiyo itasaidia wananchi kufuga kisasa zaidi, kuongeza kipato na kupunguza utegemezi wa shughuli moja ya kilimo pamoja na kuzuia vitendo vya uharibifu wa mazingira katika maeneo ya hifadhi.

Picha ya Catherine Kimario Mratibu wa Mahusiano na maisha endelevu STEP(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya Catherine Kimario-STEP

Vikundi vilivyonufaika na mafunzo hayo ambayo katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara yalizinduliwa mei 25,2026 ni pamoja na Tunza Mazingira na Misitu ni Hazina kutoka kata ya Lumemo, Wahifadhi Machipi kuta ya Michenga pamoja na Tuwarithishe kutoka Signali.

Kwa upande wake, Afisa Mifugo kutoka kampuni ya NIR Animal Trust ya Arusha, James Julius, amesema wafugaji wengi wa kuku wa kienyeji bado hawazingatii kanuni bora za ufugaji hali inayochangia kuenea kwa magonjwa.

Amesema ugonjwa wa Kideri ni miongoni mwa magonjwa hatari kwa kuku na njia bora ya kuudhibiti ni kutoa chanjo kwa wakati kabla kuku hawajaugua.

Picha ya James Julius Afisa mifugo mwezeshaji kutoka NIR Animal Trust akitoa mafunzo katika kikundi cha Tunza mazingira Lumemo (Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya James Julius Mwezeshaji-NIR Animal Trust

Naye Daktari wa Mifugo wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara Dkt.Dunia Mlanzi amewataka wananchi kuendeleza ufugaji bora wa kuku kwa kuwa ni njia muhimu ya kuongeza kipato cha familia huku akieleza kuheshimu mchango wa wadau kama STEP kupitia Polish aid kuisaidia serikali kuendeleza sekta ya mifugo ili kuinua uchumi wa wananchi.

Picha ya Dkt.Dunia Mlanzi Daktari wa Mifugo Halmashauri ya Mji wa Ifakara(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya Dkt.Dunia Mlanzi

Baadhi ya wanufaika wa mafunzo hayo kikundi cha Tunza Mazingira Lumemo wameishukuru STEP pamoja na Polish Aid wameelezea uzoefu wao katika ufugaji wa kuku wa kienyeji huku wakisema elimu waliyoipata itasaidia kuboresha maisha yao kupitia ufugaji wa kuku wa kienyeji.

Picha ya baadhi ya wanakikundi cha Tunza mazingira wakipata mafunzo ufugaji na afya ya kuku(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti za wanufaika

Tangu mwaka 2014, STEP imekuwa ikitekeleza shughuli za uhifadhi wa tembo, mazingira na utoaji wa elimu ya uhifadhi kwa jamii na kuwezesha njia mbadala ya kipato katika maeneo mbalimbali kusini mwa Tanzania .