Pambazuko FM Radio

Madereva Mang’ula watoa kero zao

14 August 2026, 08:43

Madereva wa Boda boda na bajaji wakimsikiliza Traffic WP9076 Mary Bayo – Mang’ula – picha na: Sgt Rajabu Kadikarange

Madereva wa bodaboda na bajaji Tarafa ya Mang’ula wameeleza changamoto zinazowakabili, zikiwemo taratibu za mauziano ya vyombo vya moto, TIN, vyeti vya udereva na gharama za mafunzo. Wataalamu kutoka TRA, MODS na Jeshi la Polisi wametoa ufafanuzi kuhusu masuala hayo pamoja na umuhimu wa madereva kutii sheria na maelekezo halali ya askari.

Na: Isidory Mtunda

Madereva wa bodaboda na bajaji kutoka Tarafa ya Mang’ula, Halmashauri ya Mji wa Ifakara, mkoani Morogoro, wamepata nafasi ya kueleza kero na changamoto zinazowakabili katika shughuli zao za usafirishaji, wakati wa mkutano wa mafunzo ulioandaliwa na mkuu wa kikosi cha usalama barabarani wilaya ya Kilombero, ASP Blandina Kasongwa.

Madereva wa boda boda na Bajaji wakimsikiliza Vehicle inspector Sgt Kadikarange – picha na: WP 9079 Mary Bayo

Baadhi ya madereva walioshiriki mkutano huo waliuliza kuhusu namna ya kumhusisha mwanasheria katika mauziano ya vyombo vya moto vinavyofanyika kwa njia za kawaida, uhalali wa namba za TIN zilizotolewa bila kutumia NIDA, pamoja na taratibu za kupata upya vyeti vilivyopotea. Pia waliomba ufafanuzi kuhusu gharama za mafunzo ya udereva ili waweze kujiandaa na kuboresha sifa zao za kitaaluma.

sauti za washiriki wakiuliza maswali

Akijibu maswali yaliyohusu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Afisa Msimamizi wa Kodi TRA Kilombero, Kulwa Hezron, amesema kumshirikisha mwanasheria katika mauziano ya vyombo vya moto vilivyotumika ni muhimu ili kusaidia kuhakikisha taratibu za kisheria zinafuatwa. Kuhusu namba za TIN zilizotolewa kupitia mfumo wa zamani ambao haukuhusisha NIDA, amesema wahusika wanaweza kuhuisha taarifa zao badala ya kuanza mchakato wa kupata TIN mpya.

Kulwa Hezron (mwenye suti) – TRA – picha na: WP 9079 Mary Bayo
sauti ya Kulwa Hezron kutoka TRA

Naye Mkurugenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Udereva MODS, Beatrice Lyamuya, ametoa ufafanuzi kuhusu madereva waliosoma zamani na kupoteza vyeti vyao, pamoja na taratibu na gharama za mafunzo kwa wanaotaka kusoma au kuongeza ujuzi wa udereva ili kuboresha sifa zao za kitaaluma.

Beatrice Lyamuya (aliyesimama) akitoa somo kwa madereva- picha na: WP 9079 Mary Bayo
Sauti ya Beatrice Lyamuya

Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Kilombero, ASP Blandina Kasongwa, amewataka madereva kutii maelekezo halali ya askari, ikiwemo kusimama wanapoamriwa kufanya hivyo. Amesema askari wanapaswa kufuata taratibu za kisheria katika kuwafuatilia madereva wanaokaidi maelekezo, na kusisitiza kuwa madereva wanaofanya hivyo wanaweza kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

ASP Blandina Kasongwa akitoa somo kwa madereva – kituo cha Polisi Mang’ula – picha na: WP 9079 Mary Bayo
Sauti ya ASP Kasongwa