Pambazuko FM Radio

St.Francis Hospital yatoa matibabu ya kibingwa bure Ifakara

8 June 2026, 13:06

Picha ya Madaktari bingwa kutoka Italia wakiwa na viongozi na madaktari St.Francis(Picha na Kuruthumu Mkata)

Uwepo wa madaktari hao ni fursa muhimu kwa wananchi kupata huduma za kibingwa karibu na maeneo yao, huku pia ikichangia kubadilishana uzoefu na ujuzi wa kitabibu

Na Katalina Liombechi

Wananchi wa Ifakara na maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Morogoro wamehimizwa kutumia fursa ya kupata matibabu ya kibingwa yanayotolewa bure na madaktari bingwa kutoka Italia walioweka kambi katika Hospitali ya Rufaa ya St. Francis kwa kipindi cha wiki mbili kuanzia leo, Juni 8, 2026.

Akizungumza kuhusu huduma hizo, Mkurugenzi wa Tiba wa hospitali hiyo, Daktari Winifrid Gingo, amesema madaktari hao watatoa huduma mbalimbali za kibingwa ikiwemo matibabu ya magonjwa ya pua, sikio na koo,Goita, upasuaji wa kurekebisha makovu yatokanayo na moto na ajali.

Picha ya Dkt.Winifrid Gingo Mkurugenzi wa tiba St.Francis(Picha na Kuruthumu Mkata)
Sauti ya Dkt.Gingo 1

Mengine ni Vidonda sugu,kuondoa vimbe kwenye matiti, matibabu ya magonjwa ya ngozi,upimaji wa saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake pamoja na matibabu ya jumla huduma ambazo zitatolewa bure.

Daktari Gingo amesema uwepo wa madaktari hao ni fursa muhimu kwa wananchi kupata huduma za kibingwa karibu na maeneo yao, huku pia ikichangia kubadilishana uzoefu na ujuzi wa kitabibu kati ya wataalamu wa afya wa Hospitali hiyo na wenzao kutoka Italia.

Ametoa wito kwa wananchi wenye changamoto za kiafya zinazohusiana na huduma hizo kujitokeza kwa wingi ili kunufaika na matibabu hayo ndani ya kipindi chote cha kambi hiyo.

Sauti ya Dkt.Gingo 2
Picha ya Madaktari bingwa wakijiandaa kutoa huduma katika Hospitali ya St.Francis Ifakara(Picha na Kururumu Mkata)

Baadhi ya wananchi waliojitokeza kupata huduma hizo wameeleza kuridhishwa na namna walivyopokelewa hospitalini hapo, wakisema wana matumaini ya kupata nafuu na kuondokana na magonjwa yaliyokuwa yakiwasumbua kwa muda mrefu.

Picha ya baadhi ya wananchi waliojitokeza kwenye huduma bingwa za matibabu St.Francis(Picha na Kuruthumu Mkata)
Sauti za Wananchi 3