Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
9 May 2026, 07:56

Baraza la madiwani Mlimba limeweka utaratibu maalum wa madiwani na viongozi kushiriki katika uchangiaji damu pamoja na upimaji wa afya kila wanapokutana kwenye vikao rasmi
Na Kuruthumu Mkata
Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba imeendelea kuimarisha juhudi za kukabiliana na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwa kuweka mikakati ya kuhamasisha upimaji na uchangiaji damu katika kila kipindi cha robo ya tatu ya vikao vya Baraza la Madiwani.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Mei 6, 2026, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, Mh. Martha Mkula, amesema kuwa baraza hilo limeweka utaratibu maalum wa madiwani na viongozi kushiriki katika uchangiaji damu pamoja na upimaji wa afya kila wanapokutana kwenye vikao rasmi.
Bi. Mkula amesema hatua hiyo inalenga kuhamasisha jamii kujitokeza kwa wingi katika kuchangia damu salama pamoja na kupima afya zao ili kusaidia kuokoa maisha ya watu wenye uhitaji wa damu na kudhibiti maambukizi ya UKIMWI ambapo pia ametoa wito kwa wananchi, watumishi wa umma pamoja na viongozi wa dini kujitokeza kwa hiari kushiriki katika uchangiaji damu na upimaji

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mlimba, Jamary Abduli, amesema halmashauri hiyo imeweka utaratibu wa kutoa posho kwa watu wanaojitolea kuchangia damu ili kuongeza hamasa na ushiriki wa wananchi katika zoezi hilo.

Naye Diwani wa Kata ya Mbingu amehoji kuhusu matumizi ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya mapambano dhidi ya UKIMWI, akitaka ufafanuzi wa namna fedha hizo zinavyotumika katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za afya ndani ya halmashauri hiyo.