Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
10 June 2026, 14:04

Shirika la Plan International limehitimisha shughuli zake za ufadhili wa watoto katika Wilaya ya Kilombero baada ya zaidi ya miaka 30, likiacha mafanikio makubwa katika elimu, afya, ustawi wa watoto na uwezeshaji wa jamii.
Na: Isidory Mtunda
Baada ya zaidi ya miaka 30 ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Kilombero, Shirika la Plan International limeacha alama kupitia ujenzi wa madarasa 172, nyumba 25 za walimu, ofisi 24 za walimu, ununuzi wa madawati 3,601 na ukarabati wa madarasa tisa, kabla ya kuhitimisha rasmi shughuli zake za ufadhili wa watoto wilayani humo.
Akizungumza katika hafla ya kufunga ofisi ya shirika hilo iliyofanyika mjini Ifakara, Mkurugenzi wa Plan International Tanzania, Jane Sembuche, amesema mbali na sekta ya elimu, shirika hilo limechangia maendeleo katika maeneo ya afya, maji, usafi wa mazingira na ustawi wa watoto kwa kushirikiana na serikali pamoja na jamii.

Kwa upande wake, mkuu wa miradi na Utekelezaji wa Plan International, Martha Lazaro, amesema maelfu ya wananchi wamenufaika na miradi mbalimbali iliyotekelezwa na shirika hilo, huku akisisitiza umuhimu wa jamii kuendeleza mafanikio yaliyopatikana baada ya mradi huo kufungwa.

Naye Diwani wa Kata ya Mbasa, Hadija Rashidi Kilama, amelishukuru shirika la Plan International kwa mchango wake katika maendeleo ya elimu eneo hilo. Amesema shirika hilo limechangia ujenzi wa Shule ya Msingi Mbasa, vyoo katika Shule za Msingi Maendeleo na Mbasa, pamoja na kutoa madawati na kusaidia watoto wengi waliokuwa wakifadhiliwa kupitia mpango wa watoto wa Plan.
Mmoja wa wanufaika wa ufadhili wa masomo kupitia Plan International, Rose Luvanda, amesema msaada alioupata ulimwezesha kuendelea na elimu na kufikia ndoto zake za kujiendeleza kitaaluma.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Maafisa Maendeleo ya Jamii Penina Hubert Kamafa wa Kata ya Mbingu na Esther Obedy Mtweve wa wa Kata ya Kibaoni wamelishukuru shirika hilo kwa mchango wake katika kuwawezesha watoto kutambua haki zao pamoja na kuimarisha vikundi vya wanawake kiuchumi kupitia shughuli za ujasiriamali.

Akifunga hafla hiyo, mkuu wa wilaya ya Kilombero, wakili Dunstan Kyobya, amewataka viongozi wa vijiji, mitaa na maafisa maendeleo ya jamii kubainisha miradi na wanufaika wote waliowezeshwa na Plan International ili serikali iweze kuendeleza na kulinda mafanikio yaliyopatikana kwa manufaa ya jamii.