Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
27 April 2026, 19:29

Akizindua mafunzo ya ufugaji wa kuku bora Mkuu wa Wilaya amewagiza wataalamu kuhakikisha wanawatembelea wafugaji mara kwa mara ili kuwapa ushauri wa kitaalamu pamoja na kuwawezesha kupata mikopo
Na Kuruthumu Mkata
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, leo Aprili 27, 2026, amezindua rasmi mafunzo ya ufugaji bora na salama wa kuku, akisisitiza umuhimu wa wananchi kuwekeza katika ufugaji wenye tija huku wakizingatia viwango vya usalama.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Kyobya amewahimiza wananchi wa Kilombero kujikita katika ufugaji wa kisasa wa kuku ili kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.
Aidha, ameagiza maafisa maendeleo kuhakikisha wanawatembelea wafugaji mara kwa mara ili kuwapa ushauri wa kitaalamu pamoja na kuwawezesha kupata mikopo kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao.
Katika hatua nyingine, Kyobya amesisitiza umuhimu wa wafugaji kuunda umoja wao, akieleza kuwa hatua hiyo itarahisisha upatikanaji wa huduma, mikopo na masoko huku akiwapongeza KV HELP waandaaji wa Mafunzo hayo kwa juhudi zao za kuwapa mbinu wananchi ya kujikwamua kiuchumi.

Kwa upande wake, mratibu wa mafunzo hayo yanayofanyika kwa siku nne kuanzia leo Aprili 27,2026 Katika Ukumbi wa vijana Halmashauri ya Mji wa Ifakara Idd Mayumana kutoka KV HELP, amesema wafugaji wengi wamekuwa wakipata hasara kutokana na ukosefu wa elimu sahihi ya ufugaji, hasa katika matumizi ya dawa akieleza kuwa matumizi ya dawa yasiyo sahii husababisha vifo vya kuku na kupunguza uzalishaji.

Naye Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Bi Florence Mwambene, amewahimiza wafugaji kutumia fursa za mikopo zinazotolewa na taasisi mbalimbali ili kuongeza mitaji na kuboresha ufugaji wao.
Hata hivyo, baadhi ya wafugaji walioshiriki mafunzo hayo wameiomba serikali kuhakikisha upatikanaji wa soko la uhakika kwani kwa sasa wanakabiliwa na changamoto ya masoko, hali inayowalazimu kuuza kuku kwa bei ya chini kupitia wauzaji wa kati na pembezoni mwa barabara.
