Pambazuko FM Radio
Pambazuko FM Radio
7 July 2025, 11:12

Katika juhudi za kupunguza upotevu wa mazao kwa wakulima wadogo, Shirika la Farm Africa limeendesha mafunzo ya kilimo bora kwa wakulima wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara. Kupitia ushirikiano na wadau wa teknolojia ya kilimo, mafunzo haya yamelenga kuwajengea wakulima uelewa wa mbinu sahihi za kuvuna, kupura na kuhifadhi mazao ili kuongeza tija na kipato.
Na; Isidory Mtunda
Shirika la Farm Africa limeendesha mafunzo kwa wakulima kutoka baadhi ya kata za Halmashauri ya Mji wa Ifakara, mkoani Morogoro, kwa lengo la kupunguza upotevu wa mazao—kwa kiasi na ubora.
Akizungumza na Pambazuko FM wakati wa mafunzo yaliyofanyika katika moja ya vijiji, Mratibu wa Mradi wa Farm to Market Alliance, Bw. Fredrick Akyoo, alisema zaidi ya asilimia 30 hadi 40 ya mavuno hupotea kabla hayajafika sokoni kutokana na mbinu duni za uvunaji, upuraji na uhifadhi.

Katika ziara hiyo, Farm Africa iliambatana na wadau mbalimbali wanaosaidia shughuli za kilimo, ikiwa ni pamoja na kampuni ya Poly Machinery, inayojihusisha na mashine za kilimo, ujenzi na ufugaji.
Pia walikuwepo wawakilishi kutoka kampuni ya A to Z Textile Mills Ltd, watengenezaji wa mifuko maalumu ya kuhifadhia nafaka aina ya AgroZ, ambayo huzuia hewa na hivyo kuzuia wadudu na fangasi kuathiri mazao yaliyohifadhiwa.

Mtaalamu kutoka kampuni ya A to Z Textile Mills Ltd – Picha na Tumaini Mbwambo
Naye afisa Kilimo wa Kata ya Mwaya, Bi. Neema Mhongole, amesema ujio wa Farm Africa umeongeza maarifa ya kilimo bora kwa wakulima wa eneo hilo, hasa katika nyanja za uvunaji, uhifadhi na upuraji.
Kwa upande wao, wakulima walioshiriki wamepongeza juhudi hizo na kusema kuwa vifaa vilivyooneshwa, ikiwemo mashine za kupuria na mifuko ya AgroZ, vinarahisisha kazi na kusaidia kupunguza hasara ya mazao.

picha ya wananchi wakipata maelekezo jinsi ya kutumia mashine ya kuvuna Mpunga – Picha na Tumaini Mbwambo
sauti za wananchi
Mafunzo kwa wakulima wa Ifakara yameendeshwa na Farm Africa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ya kilimo. Yalilenga kukabiliana na upotevu wa mazao unaotokana na uhifadhi usio salama na mbinu duni za kuvuna. Kwa ushirikiano na kampuni kama Poly Machinery na A to Z Textile Mills Ltd, wakulima wamepata elimu ya vitendo juu ya teknolojia mpya za kilimo. Hatua hii inalenga kuboresha usalama wa chakula na kipato cha mkulima wa kawaida.