Pambazuko FM Radio

UKICU yachagua viongozi wapya

25 May 2026, 10:02

Viongozi wa vyama vya ushirika kutoka mkoani – picha na; Jackline Jerome

UKICU imepata wajumbe watano wapya wa bodi kutoka Ulanga, Malinyi na Mlimba katika uchaguzi uliofanyika Mei 23, 2026, huku Ifakara Mji ikikosa mwakilishi baada ya waombaji wake kutokidhi vigezo.

Na: Isidory Mtunda

Chama Kikuu cha Ushirika cha Ulanga na Kilombero (UKICU) kimefanya uchaguzi wa viongozi wake Mei 23, 2026, chini ya usimamizi wa kamati ya uchaguzi iliyoongozwa na Mrajisi Msaidizi wa vyama vya Ushirika Mkoa wa Morogoro, Emmanuel Sanka, na kupata viongozi wapya watano wa bodi, mwenyekiti pamoja na makamu mwenyekiti watakaohudumu kwa kipindi cha mwaka mmoja

Sesilia Sosthenes – mrajisi msaidizi Morogoro – picha na: Jackline Jerome

Akizungumza na Pambazuko fm baada ya mkutano huo, Mrajisi Msaidizi Mkoa wa Morogoro, Sesilia Sosthenes, amesema UKICU imepata wajumbe watano wa bodi, huku Ifakara Mji ikikosa mwakilishi baada ya waombaji wake kutokidhi vigezo vya uchaguzi.

Sauti ya Sesilia Sosthenes

Baada ya uchaguzi huo, Pambazuko fm ilizungumza na mwenyekiti mpya wa bodi ya UKICU, Ritha Charles Nyela kutoka Kilosa Mpepo AMCOS, ambaye ameahidi kusimamia malipo ya wakulima wanaohifadhi mazao ghalani yafanyike kwa wakati ili kupunguza malalamiko na kuhakikisha bodi inafanya kazi kwa uwazi na weledi.

Sauti ya Ritha C. Nyela

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo, amewataka viongozi wa UKICU kuzingatia uadilifu, kuhakikisha malipo ya wakulima yanatolewa kwa wakati, pamoja na kusimamia ubora wa maghala ya kuhifadhia mazao ya wakulima.

Mkuu wa wilaya ya Kilombero wakili Dunstan Kyobya – picha na: Isidory Mtunda
Sauti ya mkuu wa wilaya ya Kilombero D. Kyobya

UKICU, inayohudumia halmashauri za Ulanga, Malinyi, Mlimba na Ifakara Mji kupitia vyama vya msingi 52 vya ushirika, imewapata viongozi wapya wa juu ambao ni mwenyekiti Ritha Charles Nyela na makamu mwenyekiti Fideli Atupele Mwakasege.