Pambazuko FM Radio

Wajane  Ifakara wapinga mila kandamizi

23 June 2026, 19:35

Picha ya Wajane wakicheza katika maadhimisho ya siku yao leo(Picha na Katalina Liombechi)

Licha ya kuamini umoja kuwa sauti yao kukabiliana na changamoto hizo wameziomba mamlaka husika kuendelea kutoa elimu ya sheria za mirathi na haki za wajane ili kupunguza vitendo vya unyanyasaji vinavyoendelea kujitokeza kwa baadhi ya watu

Na Katalina Liombechi

Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Wajane Duniani leo, Juni 23, 2026, wajane wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara wameendelea kueleza changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo, ikiwemo kutengwa na jamii, kudhulumiwa mali, kunyang’anywa watoto pamoja na kufukuzwa katika makazi yao na ndugu wa marehemu mara baada ya wenza wao kufariki dunia.

Changamoto hizo zimebainishwa na viongozi wa Chama cha Wajane katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara wakati wa maadhimisho ya siku hiyo yaliyofanyika katika Viwanja vya Bethelehem, Kata ya Kibaoni, yakihusisha wajane pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo ya jamii.

Wajane walioshiriki maadhimisho hayo wameiomba jamii kuacha mila na desturi kandamizi zinazochangia kuwanyima haki zao, huku wakizitaka mamlaka husika kuendelea kutoa elimu ya sheria za mirathi na haki za wajane ili kupunguza vitendo vya unyanyasaji vinavyoendelea kujitokeza.

Picha ya Mwenyekiti wa chama cha wajane Ifakara(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti za Viongozi wa wajane

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Afisa Ustawi wa Jamii anayeratibu masuala ya wajane Benadetha Khamsini amesema kuwa Siku ya Wajane Duniani ni fursa muhimu ya kuenzi na kutafakari mafanikio yaliyopatikana katika kuboresha maisha ya wajane, sambamba na kutambua changamoto zinazowakabili ili ziendelee kufanyiwa kazi na kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu.

Aidha amekiri ofisi yake imekuwa ikipokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa wajane, hususan yanayohusu migogoro ya mirathi, unyanyasaji wa kijamii na ukiukwaji wa haki zao, na kwamba imeendelea kutoa msaada wa kisheria na kijamii kwa waathirika ili kuhakikisha wanapata haki stahiki.

Picha ya Benadetha Khamsini Afisa Ustawi Mratibu wa Masuala ya wajane Ifakara(Picha na Katalina Liombechi)
Sauti ya Afisa Ustawi Ifakara

Maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani mwaka huu 2026 yamekuwa jukwaa la kuhamasisha usawa, ulinzi wa haki za wajane na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu mchango wao katika maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla ambayo inakwenda na kauli mbiu isemayo ”Imarisha haki utu na uwezeshaji kiuchumi kwa wajane